Wakala wa Pogba aitesa Manchester United

Muktasari:

Tangu Julai mwaka jana Raiola ana kazi moja tu kuivuruga Man United na kuna kila dalili mbinu zake zinaelekea kufanikiwa na Pogba ataondoka Old Trafford.

MANCHESTER, ENGLAND . WAKALA wa Paul Pogba, Mino Raiola ni jeshi la mtu mmoja na sasa yuko vitani na Manchester United nzima kuhakikisha anamg’oa mteja wake Old Trafford.

Tangu Julai mwaka jana Raiola ana kazi moja tu kuivuruga Man United na kuna kila dalili mbinu zake zinaelekea kufanikiwa na Pogba ataondoka Old Trafford.

Julai 5, 2019

Shida ilianzia hapa baada ya Raiola kuibuka na kusema anataka kumuuza Pogba. “Kila mtu anajua kuwa Paul (Pogba) anataka kuondoka, tuko kwenye mchakato, kila mtu anajua mawazo ya Paul. Kila mtu ndani ndani ya klabu kuanzi kwa kocha hadi wamiliki wanajua nini Paul anataka.”

Julai 10

Kocha wa Man United, Ole Gunner Solskjaer akajibu mapigo kwa kueleza klabu hiyo haina mpango wa kumuuza mchezaji, huku akisisitiza hapendi kukaa na kujibu kile kinachosemwa na Pogba na wakale wake (yaani Raiola), na mchezaji huyo ana mkataba na klabu hivyo hana hofu ya kumpoteza.

Septemba 16

Gwiji wa Man United, Gary Neville ananunua kesi na kumshukia Raiola na kusema wakala huyo anatia aibu huku akiitaka klabu yake hiyo ya zamani kuacha kufanya biashara na wakala huyo, kwa sababu alisema siku zote wakala huyo anaangalia pesa kila anapotaka kuhamisha mchezaji wake.

Desemba 30

Raiola ampiga kijimbe Solskjaer kwa kusema yeye anazungumza na Ed Woodward na si kocha huyo, huku akisema Ole akitaka kuzungumza lolote kuhusu Pogba ampigie siku kwa sababu namba yake anayo, lakini si kwenda kwenye vyombo vya habari.

Desemba 31

Siku moja ya baada ya kumpiga kijembe Solskjaer, Raiola safari hii aishukia Man United akidai Pogba anatakiwa kucheza timu inayoshinda mataji na inashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuushangaa uongozi wa klabu hiyo kwa kukaa tu bila kuchukua hatua wakati timu inazidi kupotea. Siku hiyo hiyo anaenda mbali zaidi na kusema hatampeleka mchezaji yeyote Old Trafford kwa sababu kwa sasa timu hiyo inaweza kuua kipaji hata cha Diego Maradona, Pele na Paolo Maldini.

Januari 1, 2020

Licha ya Pogba alikuwa anaweza kupona majeraha ya enka yanayomsumbua bila upasuaji, lakini Solskjaer anadai watu wa karibu wa kiungo huyo (wakiongozwa na Raiola) wamemshauri afanyiwe upasuaji.

Januari 1

Rio Ferdinand aingia vitani na kumponda Raiola, huku akisema: “Ningekuwa mtu ambaye namshauri Paul (Pogba), ningemwambia nenda kazungumze ishu zako mwenyewe usimruhusu wakala wako aongee, mfunge mdomo.”

Januari 2

Raiola aishukia tena United, akisema: “Sikumlazimisha kwa silaha mtu yeyote pale Manchester United kumsajili Paul Pogba, Alex Ferguson alinipinga mimi na Paul, hilo linaruhusiwa, lakini alikuwa wapi walipomrudisha.”

Januari 22

Solskjaer afunguka timu hiyo haikumsajili Haaland kwa sababu wakala wake Raiola, alikuwa anataka vitu vingi sana ambavyo vingeifanya Man United kukosa nguvu kwa mchezaji.

Januari 22

Raiola ampiga tena kijembe Solskjaer, akisisitiza hana mawasiliano naye na badala yake ishu zote zinazomuhusu Pogba anazungumza na bosi wa Ole, Woodward kwa sababu ndiyo mwenye sauti.

Februari 14

Safari hii kaamua kumhusisha Pogba na Juventus, huku akisisitiza Italia ni kama nyumbani kwa mteja wake na angetamani kurudi Turin na kuweka wazi anasubiri kuona nini kitatokea baada ya michuano ya Euro 2020.

Februari 15

Siku moja baadaye Raiola aweka wazi Pogba ataondoka Man United kama timu hiyo itashindwa kufuzu kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kugombea ubingwa wa Ligi Kuu England.

Februari 17

Solskjaer amshukia mazima Raiola na kusisitiza kuwa wakala huyo hana nguvu yoyote ya kuamua kama Pogba anabaki au anaondoka Old Trafford kwa sababu ni mchezaji wao na ana mkataba.

Februari 17

Dakika 17 kabla ya mechi ya Ligi Kuu England kati ya Chelsea dhidi ya Man United, Raiola anajibu mapigo kwa Solskjaer, kupitia ukurasa wake wa Twitter, akisisitiza kwamba Pogba si mfungwa na hamilikiwi na yeye wala Solskjaer na ana haki ya kuamua nini anataka kufanya, huku akimdhihaki Solskjaer kwa kusema kocha huyo amechanganywa na mambo yanavyoenda ndani ya klabu hiyo.

Februari 17

Roy Keane aitaka klabu yake ya zamani imuuze Pogba wakati wa kiangazi kwa sababu ni aibu kwa timu kubwa kama Man United kuingia kwenye vita ya maneno na wakala kama Raiola.

Februari 18

Raiola amshukia Gary Neville na kumdhihaki kwa kusema inaonekana beki huyo wa zamani wa Man United anajua sana soka, lakini anashangaa kwa nini timu yake anayomiliki pamoja na wachezaji wenzake wa zamani wa United, Salford City haipandi daraja.

Februari 18

Neville ajibu mapigo kwa kumwita Raiola chawa, huku akidai maneno yake hayamsumbui na kudai kuwa anaona kuna kila dalili kelele za Pogba kuondoka Man United kuisha wakati wa kiangazi na kwamba hamuoni staa huyo akiwa kwenye kikosi cha United msimu ujao.