Wakala wa Kakolanya ashangaa kipa huyo kupelekwa Simba

Muktasari:

  • Kipa wa Yanga, Beno Kakolanya tangu arejee na kikosi cha timu ya Taifa kilipokwenda kucheza na Lesotho hajajiunga na klabu yake akishinikiza kulipwa madeni yake ya fedha za usajili na mishahara.

Dar es Salaam. Meneja wa kipa Beno Kakolanya, Seleman Haroub ameweka wazi msimamo wake na mchezaji huyo kwamba hakuna jambo linalomalizwa kienyeji kama watu wanavyochukulia ishu ya mchezaji wake na Yanga na kwamba ikifikia hatua ya kuvunja mkataba basi watafuata taratibu zote.

Kakolanya anayeichezea Yanga anaidai klabu hiyo fedha za usajili pamoja na mishahara, madai ambayo yamepeleka ashindwe kujiunga na kikosi chake ambacho leo Jumatatu jioni kitakuwa na kibarua dhidi ya Prisons kwenye uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Habari ambazo zilienezwa kwenye mitandao ya kijamii ni kwamba kipa huyo kutaka kuondoka Yanga na kujiunga na watani zao Simba, taarifa ambazo Haroub amesema hazipo na hakuna barua yoyote iliyoandikwa.

"Watu hutengeneza maneno, nafahamu taratibu za kudai maslahi ya mchezaji, hatuwei kukurupuka tu na kwenda TFF (Shirikisho la Soka nchini) kupeleka madai yetu, kinachotakiwa kufanywa tena kwa weledi mkubwa ni kufanya mazungumzo na Yanga ambapo tumefanya kwa mdomo.

"Baadaye ndipo tutafikiria kuandika barua ya kupeana muda wa kulipa madeni hayo ambapo barua hiyo kopi yake itakwenda TFF, tukiona mambo bado magumu ndipo tutaandika barua moja kwa moja TFF ya kuomba msaada, huo ndio utaratibu na si vinginevyo.

"Sisi sote ni familia moja ya mpira, tunafahamu hali halisi ya uchumi ndani ya Yanga ingawa hatumaanishi kwamba wasitulipe, hakuna mpango wowote wa Beno kuja Simba na siwezi kufanya hivyo, sitakuwa muungwana kwani hatujachukuwa hatua yoyote ya kudai kiofisi kwa maana ya kuwaandikia barua," alisema Haroub ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba upande wa klabu.

Wakati Haroub akiweka wazi juu ya hilo, TFF nayo imekanusha juu ya taarifa hizo zilizozagaa mitandano kwamba hakuna kikao chochote kilichokaa cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kujadili suala hilo.

Katika taarifa hizo zilizokuwa zimesambaa zilieleza kwamba Kamati hiyo imethibitisha kwamba Kakolanya ni mchezaji huru baada ya Yanga kushindwa kumlipa madeni yake ambayo ni pesa ya usajili na mishahara.