Wakala: Ozil Arsenal ndio keshafika hivyo

Muktasari:

Ozil ni mchezaji namba 5 katika chati ya wachezaji wanaovuta mkwanja mrefu zaidi kwenye Ligi Kuu ya England na anawaacha mbali sana wachezaji wenzake kikosini Arsenal kwa mshahara mkubwa, lakini amecheza mechi 23 tu katika michuano yote msimu huu.

LONDON, ENGLAND . WAKALA wa kiungo wa Arsenal, Mesut Ozil amesisitiza kwamba mteja wake “ana zaidi ya furaha” klabuni hapo na anapachukulia London Kaskazini kama “nyumbani” kwake.

Ozil ni mchezaji namba 5 katika chati ya wachezaji wanaovuta mkwanja mrefu zaidi kwenye Ligi Kuu ya England na anawaacha mbali sana wachezaji wenzake kikosini Arsenal kwa mshahara mkubwa, lakini amecheza mechi 23 tu katika michuano yote msimu huu.

Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani amekuwa akipata nafasi mara kwa mara ya kucheza katika kikosi cha kwanza tangu Mikel Arteta achukue kiti kilichoachwa na Unai Emery, na wakala wake, Erkut Sogut amebainisha kuwa Ozil amevutiwa na uongozi wa bosi wake mpya.

“Nadhani (Mikel) Arteta ni kocha mzuri sana na amejifunza kutoka kwa makocha bora duniani.

Alifanya kazi na Pep Guardiola kwa miaka mingi na nadhani anajua anachokifanya,” Sogut alisema.

“Ozil ana zaidi ya furaha pale Emirates Stadium. Anaipenda klabu, anawapenda mashabiki na anaupenda mji. Huu ni mwaka wake wa saba akiwa na Gunners na anapenda kuwa sehemu ya jamii ya Arsenal. Pale ni nyumbani kwake.”

Ozil ameanza katika mechi zote 10 zilizopita za Arsenal kwenye Ligi Kuu ya England.