Waingereza waweka dau kimya kimya kwa Ivan Rakitic

Muktasari:

Barcelona wapo tayari kuachana na Rakitic dirisha la Januari tu baada ya staa huyo kupoteza nafasi yake kwa kinda Frenkie de Jong aliyewasili klabuni hapo akitokea Ajax dirisha kubwa lililopita la majira ya joto.

BARCELONA imekataa ofa kutoka katika klabu moja ya Ligi Kuu ya England iliyokuwa inamtaka staa wao wa kimataifa wa Croatia, Ivan Rakitic, 31 kwa dau la pauni 13 milioni ikiwa ni pungufu ya pauni 17 milioni kwa bei waliyopanga kumuuza.

Wababe hao wa Hispania wanataka Pauni 30 milioni kwa ajili ya kumuuza nyota huyo ambaye hana nafasi katika kikosi cha kwanza Nou Camp na inadhaniwa Manchester United ndio inayomfukuzia staa huyo.

Barcelona wapo tayari kuachana na Rakitic dirisha la Januari tu baada ya staa huyo kupoteza nafasi yake kwa kinda Frenkie de Jong aliyewasili klabuni hapo akitokea Ajax dirisha kubwa lililopita la majira ya joto.

Man United imekuwa kwenye harakati za kutaka kurudisha makali yake kutokana na hali iliyoko kikosini mwao, huku Kocha Ole Gunnar Solskjaer akikabidhiwa kitita kwa ajili ya kufanya usajili wa maana dirisha la Januari.