Wadau wachekelea kiingilio bure Kenya vs Ethiopia

Muktasari:

Awali shirikisho la soka nchini (FKF), ilitangaza viingilio vya mchezo wa marudiano kati ya Harambee Stars dhidi ya Ethiopia kuwa ni Sh200 kawaida na Sh1000 VIP.

Nairobi, Kenya. Siku moja baada ya serikali kupitia wizara ya michezo, kutangaza kuwa hakutakuwa na kiingilio chochote kwa wote wataotaka kuishangilia timu ya taifa, Harambee Stars, itakapokabiliana na Ethiopia, katika uwanja wa Taifa wa Moi Kasarani, Jumapili hii.

Harambee Stars iliyolazimisha sare ya 0-0, na Ethiopia kwenye Uwanja wa Bahir Dar, itajitosa uwanjani Kasarani kwa lengo la kusaka ushindi huku matumaini makubwa wakiyaelekeza kwa mashabiki ni mchezaji namba 12.

Stars inayonolewa na Mfaransa Sebastien Migne kwa sasa inaongoza kundi F, kama watafanikiwa kushinda mchezo wa Jumapili, watakuwa na uhakika wa kufuzu kombe la mataifa Afrika, kwa mara ya kwanza tangu wafanye hivyo mwaka 2004.

Kupitia kwa waziri mwenye dhamana wa michezo, Rashid Echesa, serikali iliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushangilia timu ya taifa, na kuwapa morali ya kushinda mtanange huo muhimu.

Kufuatia uamuzi huo, wadau wa soka kupitia mitandao ya kijamii wameonesha kufurahishwa na ketendo hicho huku wakiiomba FKF, kuhakikisha kila shabiki anatinga jezi za Stars siku ya mchezo.

Wakiongozwa na shabiki namba moja wa Gor Mahia, Jaro Soja, wadau wa soka kupitia ukurasa wa ‘KPL Chat’, kwenye Facebook, walisema uamuzi huo utasaidia kuingozea Stars morali huku wakitamba kuwa lazima wahabeshi wafe.

“Kwa mara ya kwanza, tunashuhudia serikali ikifanya jambo la kizalendo katika michezo. Harambee Stars inahitaji sapoti yetu, Tuna nafasi ya kwenda Cameroon, game ikiwa sare, ni poa juu wengi wataenda graoo,” alisema Jaro Soja.

Hata hivyo, macho na masikio yameelekezwa kunako ofisi za FKF, kwani kufutwa kwa viingilio ni pigo kwao kwa sababu hiyo inamaanisha kuwa watakosa pesa inayotokana na viingilio ambayo ni kati ya shilingi 3-5 milioni.