Wadau wa soka waunga mkono Eymael kutimuliwa

Muktasari:

Kocha Eymael amezua gumzo kwa wadaui wengi wa michezo kutokana na kauli yake ya ubaguzi aliyoitoa kwa mashabiki wa klabu hiyo.

BAADHI ya wachambuzi na wachezaji wa zamani wa soka hapa nchini wameunga mkono uongozi wa Yanga kumtimua kocha wao Luc Eymael kutokana na kauli za kibaguzi.

Jana Jumapili, kwenye mitandao ya kijamii ilisambaa sauti ya kocha huyo ikitoa maneno ya kibaguzi kwa mashabiki wa klabu hiyo na kuzua mjadala mkubwa kwa wadau wengi wa michezo.

Tayari uongozi wa Yanga kupitia Kaimu Katibu mkuu, Simon Patrick umetoa taarifa kwa vyombo vya habari ya kumfuta kazi kocha huyo na pia kuwaomba radhi viongozi wa  nchi, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kwa kitendo hicho cha ubaguzi alichokitoa Eymael.

Pia TFF kupitia Ofisa Habari wake, Cliford Ndimbo imesema itamfikisha Eymael kwenye vyombo husika kutokana na matamshi yake ya kibaguzi vile vile itawasilisha Shirikisho la Kimataifa la mpira wa miguu (FIFA) kuhusu kauli hizo ili limchukulie hatua.

"Uongozi wa Yanga umesikitishwa na kauli zisizo za kiungwana na kibaguzi, tumemfuta kazi na tunahakikisha ataondoka nchini haraka iwezekanavyo," imesema taarifa hiyo.

Mchambuzi Ally Mayay, amesema kauli aliyoitoa Eymael sio nzuri kwani ameichafua taswira ya klabu.

"Tetesi za Yanga kuachana na kocha zilikuwepo hata kabla ya hiyo kauli ya kocha  kutoka hivyo ni kama kauli yake imechagiza kuharakishwa kwa uamuzi wa viongozi kumtimua.

"Eymael amekosea sana kwani kutoa siri au madhaifu ya familia yako  sio kitu kizuri maana inaharibu taswira ya klabu na hata mwenyewe inamuharibia. Imeonyesha kwa kiasi fulani alivyo na mapungufu ya kimaadili kama kocha", amesema Mayay.

Naye kiungo wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua, Yanga haijakosea kumtimua Eymel kutokana na kauli yake hiyo ya kibaguzi.

"Ubaguzi unapingwa duniani kote hivyo uongozi wa Yanga umefanya jambo zuri na la maana kumtimua kwa sababu Eymael alikuwa na matatizo mengi nyuma ya pazia ambayo mashabiki walikuwa hawayajui na viongozi walikuwa wakikaa kimya tu hivyo kwa sasa nafikiri wamechoshwa na mambo yake" amesema Chambua.