Wadau: Yanga mkiwa na matokeo Kaze hatadumu

Dar es Salaam. Makocha na wachezaji wa zamani wamewataka mashabiki na uongozi wa Yanga kumpa muda na kumuacha kocha mpya Cedric Kaze afanye kazi, lakini endapo watakwenda na matokeo viwanjani basi hatadumu ndani ya klabu hiyo.

Kaze alitua nchini Alhamis iliyopita usiku kuchukua mikoba ya Zlatko Krmpotic aliyetimuliwa mwezi uliopita kutokana na kile kilichodaiwa timu haichezi soka la kuvutia licha ya kupata ushindi katika mechi.

Kocha mpya raia wa Burundi aliyesaini mkataba wa miaka miwili atakuwa na kazi ya kuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo iliyokosa ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo.

Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima alisema Kaze ni mmoja wa makocha wazuri wanaolifahamu soka la Afrika, hivyo kama atapewa muda na ushirikianao ataifanya kuwa tishio.

Malima alisema kocha huyo ameonyesha alikuwa anaifuatilia Yanga muda mrefu, hivyo anaweza kuisaidia, lakini anatakiwa kuanza kuwajenga wachezaji kisaikolojia ili waendelee kupambana kupata ushindi.

“Timu ilikuwa inafanya vizuri, lakini kocha akaondolewa, hivyo inaweza kuwaathiri wachezaji, huyu kocha mpya anatakiwa kwanza kuwajenga kisaikolojia kwanza kujua ni jambo la kawaida ili waendelee kupambana na kupata ushindi mechi zijazo,” alisema.

“Kingine viongozi na mashabiki wanatakiwa kumpa muda kocha ili afanye kazi yake vizuri na kuitengeneza timu kama vile anavyotaka na jinsi mashabiki wanataka soka lichezwe.”

“Wasiende na matokeo yao uwanjani, bali wanatakiwa kuwa wavumilivu, wamsapoti kocha na kumpa muda wa kuijenga timu na baadaye itacheza soka la burudani kama wanavyotaka.”

Kocha mkongwe Mrage Kabange alisema Kaze anatakiwa kujua matamanio makubwa ya mashabiki wa klabu hiyo ni timu kutocheza soka la burudani uwanjani licha ya kwamba inashinda mechi, hicho ndicho kitu anatakiwa kuanza nacho.

“Nafikiri amekuwa akifutilia soka la Tanzania na hata timu aliyoenda, hivyo anajua kuwa wanataka nini, ni kitu ambacho anatakiwa kuhakikisha kinakuwa cha kwanza ili kupata ushindi katika mechi na hata kuwafurahisha mashabiki wa klabu hiyo,” alisema.

“Pia mashabiki nao waache nongwa, haiwezekani kocha anafika tu basi wanataka timu icheze soka wanalotaka wao, hiyo haipo duniani mpira sio kama chumvi kwamba muda huo huo ukiweka inakolea, lazima ichukue muda. Hivyo ndio kwanza amefika anatakiwa kupewa muda hata mechi saba hivi ndio waanze kuhoji.”

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema kikubwa ambcho kocha huyo anatakiwa kujua ni kwamba ana mzigo mkubwa wa matarajio ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo ambao wanaamini msimu huu wamesajili wachezaji wazuri.

“Mashabiki, wapenzi na wanachama wa Yanga wanaamini msimu huu wamesajili kikosi kizuri, hivyo timu yao inastahili kucheza soka zuri na kupata ushindi, huo ni mzigo kwa kocha Kaze kutimiza matarajio hayo,” alisema Mayay.

“Hata hivyo hataweza kuingiza vitu vipya kwa haraka, hivyo atategemea ushauri mkubwa kutoka katika benchi la ufundi akiongozwa na kocha msaidizi Juma Mwambusi anatakiwa pia kusikiliza ili kwenda vizuri.

“Pia katika kutafuta taarifa mbalimbali anatakiwa kuwa na vyanzo vingi ikiwemo hata mashabiki ili anapofanya uamuzi wa wachezaji wake afanye kwa akili kwani siku likitokea la kutokea yeye ndiye anayewajibika.”

Wakati akisaini mkataba na Yanga juzi, Kaze alisema: “Nina muda mfupi wa kufanya mazoezi na timu na kuingiza vitu vipya kabla ya mchezo wangu wa kwanza wa Ligi Kuu kama kocha wa Yanga, lakini kuna mambo ya msingi zaidi ya kuanza nayo.