Wadau: Kocha Yanga kaonewa

KITENDO cha uongozi wa Yanga kumfungashia virago kocha wao Mkuu Zlatko Krmpotic raia wa Serbia, kimepingwa na wadau huku wakiwataka viongozi kuheshimu taaluma.

Ikumbukwe Zlatko alitua Yanga wiki moja kabla ya Ligi Kuu Bara kuanza kutimua vumbi Septemba 6, mwaka huu na amedumu kwa siku 35 pekee, pia hakuweza kufanya usajili ndani ya timu hiyo.

Zamoyoni Mogella, mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars alisema; “Sio sahihi kabisa, timu haikuwa na muunganiko kabisa, kumbuka huyu kocha hajafanya usajili wala nini alitakiwa kuwa na muda wa kuwajua vizuri wachezaji wake, cha msingi washukuru alikuwa akipata matokeo.” “Hili ndilo soka letu la Kibongo sijawahi kuona kocha amekaa zaidi ya misimu mitatu makocha wetu akijitahidi msimu mmoja na nusu anatimuliwa, wakati walau misimu mitatu unaweza kuona mapungufu, yote kwa yote soka limevamiwa na watu sio wa mpira wanaangalia matumbo yao na sio soka,” alisema Mogella.

Huku Kocha Choke Abeid alisema; “Timu ina wachezaji wapya mwalimu mpya, kwake mwalimu kila kitu kilikuwa kipya kwake, tunaona Simba wamefanya vizuri baada ya kumpa nafasi kocha, Yanga wanaona joto kutoka kwa mashabiki kipindi kifupi sana wangemwacha.”

“Kusimamia mpira sio kazi nyepesi, sisi tunajua jamani, ila presha ya hizi timu mbili inapelekea makocha kufukuzwa tu kwa mihemko, mimi nawashauri Yanga wawe na malengo yao waache kufuata wanachokifanya Simba uwanjani, wao washukuru kupata matokeo hayo.”

Mchambuzi mahiri wa soka nchini, Alex Kashasha alisema, “Tatizo katika soka la Tanzania maamuzi hayazingatii taalumu za watu, presha pia inawafanya viongozi kufanya maamuzi, yawezekana uongozi hawakuona kile walichokitarajia, ila ulitakiwa ujue timu haikuwa na mtu wa kusajili. Kama angekaa na timu na kufanya usajili kwa muda angeweza kufanya vizuri, ila huyu kocha wamemwonea, wachezaji wameletwa tu na GSM sijui ni mapendekezo ya nani, mwalimu alikuwa mtu wa mwisho kuingia kambini Yanga, sijaona kosa lake la kufukuzwa,” alisema Kashasha

Yanga imecheza mechi tano mpaka sasa, ikishinda nne baada ya kuwafunga Kagera Sugar bao 1-0, Mtibwa Sugar bao 1-0, Mbeya City bao 1-0, Coastal Union mabao 3-0 huku akitoka sare bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons.