Wachovu: Wamechezea vichapo vya maana TPL

Saturday January 12 2019

 

By YOHANA CHALLE

UTAMU wa mechi ni mabao asikuambie mtu! Nani anafurahia suluhu kwenye mchezo? Bao liwe la sekunde za majeruhi au la mapema ni shangwe tu unaambiwa.
Wakati Ligi Kuu Bara ikiwa inajikongoja mdogomdogo huku Simba ambaye leo Jumamosi anatupa karata yake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa ndio ina viporo kibao hadi sasa.
Mnyama akiwa anajipapasa baada ya miaka mingi kupita bila kutinga hatua hiyo, huku kwenye Ligi Kuu ni moja ya timu zilizogawa vichapo vya maana kwa wapinzani wake kama Mwanaspoti linavyokuletea.

YANGA 4-3 STAND UNITED
Ulikuwa mchezo wa kutoana jasho sio mchezo kwa watoto wa Kocha, Mwinyi Zahera kwani hawakuamini kama wameondoka na pointi tatu katika mchezo huo uliopigwa Septemba 16.
Ndio mchezo ulioozaa hat trick ya Kwanza kwenye Ligi Kuu baada ya kumalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa maboa 4-3, huku Alex Kitenge aliyekuwa mshambuliaji wa Stand akitupia zote tatu.
Ulikuwa mchezo wa kwanza kwa kipa wa Yanga, Klaus Kindoki ambaye alilaumiwa vilivyo na mashabiki wa timu hiyo japo kocha alimkingia kifua.

SIMBA 5-1 ALLIANCE FC
Dakika ya tisa tu, Emmanuel Okwi aliwanyanyua mashabiki wa Msimbazi katika mchezo huo aliofunga mabao mawili. Mabao mwengine yalifungwa na Asante Kwasi, Clatous Chama na Adam Salamba.
Wakati Simba wakiamini wataondoka katika mchezo huo bila nyavu zao kuguswa, lakini Zabona Khamis aliweza kuipatia bao la kufutia machozi Alliance.

RUVU SHOOTING 0-5 SIMBA
Hat trick ya pili ya Ligi Kuu iliandikwa na Emmanuel Okwi katika mchezo huo huku Meddie Kagere na Adam Salamba wakinogesha ushindi huo kwa kila mmoja kutupia bao moja moja.
Ulikua mchezo wa pili mfululizo kwa Simba kuvuna ushindi mnene kwani wiki moja kabla ya kuichapa Ruvu walikuwa wamiilaza Alliance FC mabao 5-1.

MTIBWA 4-0 RUVU SHOOTING
Wiki mbili za mwisho wa mwezi Oktoba ulikuwa mbaya kwa Ruvu Shooting kwani walikua wametoka kupokea kichapo cha maboa 5-0 dhidi ya Simba lakini ghafla wakalala tena kwa kichapo hicho mbele ya Mtibwa na kufanya nyavu zao kuguswa mara tisa katika michezo miwili.

MBEYA CITY 4-1 AFRICAN LYON
Ndio ushindi mnono ambao Mbeya City wameweza kuuvuna hadi sasa kwenye Ligi Kuu, Desemba mbili wakiwa katika Uwanja wa nyumbani wa Sokoine waliinyeshea African Lyon mvua ya maboa 4-1 japo nao hali yao sio njema.

AZAM 4-0 MBAO
Kwa sasa Mbao FC hawajatulia kabisa kwenye kikosi chao kiasi cha kuanza kufumua benchi lao la ufundi ili kuweka mambo sawa hasa baada ya kuondoka kwa aliekuwa Kocha Mkuu Amri Said.
Walikutana na dhahama ya mabao hayo wakiwa ndani ya Dimba la Azam Complex kwa kazi nzuri ya Joseph Mahundi aliyetupia mabao mawili, Aggrey Morris, na Salum Abubakar 'Sure Boy.

KMC 5-1 PRISON
Mpaka sasa vichapo vya mabao matano ndio vimekuwa vikubwa zaidi kwenye Ligi Kuu, hivyo Prison nayo imekuwa timu ya tatu kupokea kichapo cha namna hiyo baada ya Alliance FC na Ruvu Shooting kupokea kutoka kwa Simba.
KMC ndio timu pekee kati ya timu zilizopanda msimu huu kuvuna ushindi mkubwa na kuwa miongoni mwa timu zilizofanya vyema, japo safu yake ya beki inaonekana kutokuwa imara kwani imeruhusu mabao 20.

MWADUI 4-0 KAGERA SUGAR
Kocha wa Kagera, Mecky Maxime na vijana wake wameanza mwaka mpya vibaya baada ya kupokea kichapo hicho wakiwa kwenye dimba la Mwadui Complex.
Salum Aiyee naye aliandika hat trick yake kwenye mchezo huo na kufanya hadi sasa kuwa na hat trick tatu kwenye Ligi Kuu, nyingine ikiwa ile ya Alex Kitenge pamoja na Emmanuel Okwi. Bao lingine lilifungwa na beki, Richard Mgunga.

Advertisement