Van Persie, Figo, Sterling wamehamia timu za wapinzani kisa ubingwa tu

Muktasari:

Wapo wachezaji waliohamia kwa wapinzani wa timu yao na kuwafanya kuhesabiwa kama wasaliti na kuchukiwa kwa kiasi kikubwa na mashabiki wa zamani wa timu zao.

LONDON, ENGLAND. KIPENZI cha mashabiki, nahodha na hadhi ya kufanywa gwiji kwenye klabu yake, lakini vyote hivyo unapiga teke kwa ajili ya kwenda kubeba mataji.
Kwenye soka kuna wachezaji waliamua kupiga kibuti mambo yote matamu na kuamua kutimkia timu nyingine kwa ajili ya kusaka ubingwa tu.
Hata hivyo, wapo waliohamia kwa wapinzani wa timu yao na kuwafanya kuhesabiwa kama wasaliti na kuchukiwa kwa kiasi kikubwa na mashabiki wa zamani wa timu zao.
Hawa hapa masupastaa wenye majina makubwa kwenye soka ambao waliamua kuhamia kwa mahasimu wao kwa sababu ya kutaka mataji tu.

Robin van Persie (Arsenal kwenda Man United, 2012)
Robin van Persie alikuwa nahodha na mtambo wa mabao Arsenal. Alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa kulipwa huko England na kila kitu kilionekana kuwa kizuri kwake kwenye kipindi chake alichokuwa Arsenal isipokuwa kubeba mataji tu.
Manchester United wakaja, wakiwa na mataji yao 12 ya Ligi Kuu England na hawana mtu wa maana kwenye fowadi yao. Van Persie aliamua kuwatosa Arsenal na kwenda kujiunga na United kwa ada ya Pauni 24 milioni kwa dhamira moja tu kwenda kubeba mataji. Straika huyo wa Kidachi alikwenda kufunga mabao huko United na kufanikiwa kubeba taji la Ligi Kuu England kwenye msimu wake wa kwanza tu Old Trafford na hivyo mpango wake ukakamilika.

Sol Campbell (Tottenham kwenda Arsenal, 2001)
Hebu fikiria wakati huo Arsenal ilipokuwa ikibeba mataji na kucheza soka la kibabe chini ya kocha wao Arsene Wenger.
Wachezaji wengi walitamani kwenda kuchezea timu hiyo, hata wale wa kutoka kwa mahasimu wao wakuu, Tottenham Hotspur. Hilo lilikuja kuthibitishwa na beki wa kati, Sol Campbell, aliyekuwa moto kabisa huko Spurs, lakini aliona si kitu kuamua kuhamia kwa mahasimu wao, Arsenal. Campbell aliitwa msaliti na mashabiki wa Spurs, lakini hakujali kitu kwani alikwenda kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England akiwa na Arsenal ile iliyocheza msimu wote bila ya kupoteza mchezo wowote.

Gonzalo Higuain (Napoli kwenda Juventus, 2016)
Napoli ilibahatika kuwa na straika anayefanya kazi moja tu ya kufunga mabao, Gonzalo Higuain. Straika huyo wa Kiargentina alifunga mbao 71 katika mechi 104 za ligi na alisaidia Napoli kumaliza msimu wa 2015-16 wakiwa nafasi ya pili huko kwenye Serie A.
Lakini, shida ilikuja kwenye sehemu moja tu, Napoli haikuwa na uwezo wa kushinda mataji na timu iliyokuwa na uwezo wa kufanya hivyo ni Juventus.
Gonzalo hakuona jambo jingine la kufanya zaidi ya kwenda kujiunga na Juventus, ambayo ilikuwa imebeba mataji matano mfululizo ya Serie A kwa wakati huo.
Akaenda kubeba mataji mawili ya Serie A na baada ya kutolewa kwa mkopo mara mbili, AC Milan na Chelsea, sasa amerudi tena kwenye timu hiyo akifukuzia taji jingine ya Serie A.

Luis Figo (Barcelona kwenda Real Madrid, 2000)
Kuna baadhi ya wachezaji wanahama kwa sababu kwenye mioyo yao wanafahamu wazi timu zao wanazochezea kwa wakati huo hazina uwezo wa kushinda mataji.  Lakini, Luis Figo alishinda La Liga mara mbili akiwa na Barcelona, lakini bado aliamua kuhamia Real Madrid. Ukweli kuna baadhi ya uhamisho kwamba hauwezani kusamehewa. Hata hivyo, Barcelona hawakushtuka sana kwasababu Figo alipohama Nou Camp hakumwaacha Nicklas Bendtner, alimwaacha Rivaldo, hivyo kila kitu kilikuwa sawa tu. Real Madrid walifanya hivyo kutimiza mpango wao wa kusajili mastaa wenye majina makubwa na Figo alihamia huko kwenda kutimiza lengo lake la kushinda Balon d’Or.
Tangu wakati huo, Figo hajawahi kuwa kipenzi cha mashabiki wa Barcelona na alizomewa mara zote na kurushiwa vitu aliporejea Nou Camp.

Robert Lewandowski (Dortmund kwenda Bayern Munich, 2014)
Hii kitu imekuwa tofauti. Robert Lewandowski alikuwa tayari ameshabeba mataji mawili ya Bundesliga akiwa na Borussia Dortmund, lakini hilo hakuona kama limenoga kwenye maisha yake kwa kubeba Bundesliga akiwa hayupo kwenye kikosi cha Bayern Munich.
Staa huyo aliona kwamba Dortmund hawana uwezo wa kushinda taji jingine, hivyo akaamua kwenda kujiunga na Bayern Munich.
Fowadi huyo wa kimataifa wa Poland hakujali kitu kuhusu hadhi yake huko Dortmund na kuamua kwenda kujiunga na mahasimu wao Bayern kwa ajili ya kushinda mataji zaidi.
Hatimaye, Lewandowski alikwenda kushinda mataji ya kutosha akiwa na Bayern na kujijengea hadhi kubwa kwenye kikosi hicho cha Allianz Arena.

Raheem Sterling (Liverpool kwenda Man City, 2015)
Raheem Sterling alijiunga na Liverpool akiwa kijana mdogo sana na alianza kuitumikia timu hiyo ya Anfield akiwa na umri wa miaka 17 tu.
Alikuwa mchezaji kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo na alipendwa zaidi wakati alipokuja kuunda safu matata kabisa ya ushambuliaji sambamba na wakali wengine, Luis Suarez na Daniel Sturridge.
Hata hivyo, Liverpool haikuwa na maajabu kwenye ligi, ikamaliza msimu ukiwa nafasi ya sita. Akiwa na umri wa miaka 20 tu, Sterling alipewa ofa ya mshahara wa Pauni 100,000 kwa wiki ili abaki Liverpool, lakini akakataa ili tu kwenda kujiunga na Manchester City kutimiza ndoto zake za kwenda kubeba mataji.
Hatimaye, akanaswa kwa dau lililoripotiwa kuwa ni Pauni 49 milioni. Tangu wakati huo, Sterling ameshinda mataji mwili ya Ligi Kuu England na Liverpool bado wanaendelea kusubiri kulibeba taji hilo hadi sasa.