Wachezaji wafundwa kuhusu Stars

Muktasari:

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni aliwafunda wachezaji wanaotegemewa ndani ya kikosi hicho kujitunza viwango vyao wakijua mbele yao wana jukumu la kulibeba taifa.

TAIFA Stars inatarajia kwenda kupeperusha bendera ya Tanzania huku Misri kwenye michuano ya AFCON, itakayoanza Julai, hilo limewafichua watalamu wa soka kutoa ushauri kwa wachezaji ambao ndio wahusika wakuu wa jambo hilo.
Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni aliwafunda wachezaji wanaotegemewa ndani ya kikosi hicho kujitunza viwango vyao wakijua mbele yao wana jukumu la kulibeba taifa.
Alifafanua kauli yake kwamba kuelekea kumaliza msimu huu, wachezaji wanapaswa kutumia vyema mechi zao ili ziwasaidie kuwajenga kiakili, utamamu wa mwili na kuepuka majeraha yasio na sababu.
"Kujitunza kwa wachezaji kuna maana kubwa hasa kuelekea kulibeba taifa kwenye historia ya michuano mikubwa, wachezaji wametumika muda mrefu na ligi, hivyo wanapomaliza ni wepesi wakajisahau na kutoka kwenye ari ya mchezo.

"Naamini makocha walionao watawasaidia kuwajenga kisaikolojia namna ya kujiweka tayari kwa ajili ya kulitumikia taifa kwani wachezaji ambao wanategemewa ndio hao hao wanaocheza ligi kuu"alisema.
Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula alisema wachezaji ambao wameitwa kwenye timu ya taifa wanapaswa kutanua akili zao na sio kusubiri kuingia kwenye kambi chini ya kocha wao Emmanuel Amunike ndio waanze kujiandaa.
"Tunapozungumzia maandalizi kwanza yaanzie kwenye akili ya mchezaji mwenyewe, kama kujilinda na majeraha, kuwa na nidhamu ya hali ya juu na mwili wake kwani ndio unaotegemea kufanya kazi kwa kusaidiana na akili.
"Watumie mechi za ligi kujiweka sawa na wasiwe watu wa kusubiri kujipanga wakiwa kambini na kocha wa taifa, ligi wanaocheza waitumie kwa manufaa ya kujiweka sawa"alisema.
Mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga ambaye kwa sasa ni kocha wa kikosi B cha Wanajangwani, Said Maulid 'SMG' naye alitoa lake la moyo kwamba wachezaji wakijiandaa akili zao kwenda kufanya kitu itafanikiwa.
"Kila jambo nikuliwekea nia, mfano mzuri ni Mtanzania Mbwana Samatta ambaye anafanya makubwa huku Ulaya mpaka ametwaa tuzo ya heshima ya mchezaji wa Kiafrika, aliamini kama anaweza na akaweza, hivyo Stars iamini inaenda kufanya kitu na sio kushindwa, hilo linaanzia kwa wachezaji wenyewe.