Wachezaji wa mwisho kupiga hat-trick kwa kila timu England

Muktasari:

Staa huyo wa Scotland alisajiliwa na Brighton kwa ada iliyoweka rekodi wakati huo, Pauni 35,000 kutoka Rangers na alionyesha thamani yake kwa kufunga hat-trick kwenye mechi dhidi ya Coventry, Oktoba 1980.

LONDON, ENGLAND

KUNA mtu anaitwa Diogo Jota, unamjua? Ni hivi, Jumamosi iliyopita kwenye Ligi Kuu England kulipigwa mechi moja matata kabisa, Wolves walikipiga na Leicester City, matokeo kwenye mechi hiyo ubao ulisomeka 4-3, Wolves wakifanya yao, lakini huyo mtu anayeitwa Diogo Jota, ndiye aliyefanya yake kibabe.

Diogo Jota alipiga hat-trick kuwapa Wolves pointi zote tatu. Kitendo hicho kinamfanya Jota kuwa mchezaji wa kwanza wa Wolves kufunga mabao matatu kwenye mechi moja ya ligi tangu mwaka 1977.

Lakini, unataka kujua kwenye klabu za Ligi Kuu England ni mchezaji gani wa mwisho kuondoka na mpira nyumbani kwa kila klabu za ligi hiyo, Ligi Kuu England au ile ya wakati ule ilipokuwa ikifahamika kama Ligi Daraja la Kwanza? Basi hawa hapa mastaa waliopiga hat-trick za mwisho kwenye klabu zilizopo kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

 

Arsenal - Ramsey vs Everton (2018)

Kwenye kikosi cha Arsenal mchezaji wa mwisho kufunga hat-trick ni Aaron Ramsey. Kwa bahati mbaya, kiungo huyo wa Wales mwisho wa msimu huu atakwenda kujiunga na Juventus na kama hakutakuwa na mchezaji mwingine wa Arsenal atakayepiga tatu kwenye mechi moja, basi itakuwa aibu kubwa kwenye kikosi hicho kutokana na kuwa na washambuliaji matata kabisa kama vile, Alexandre Lacazette na Pierre-Emerick Aubameyang. Ramsey alifunga hat-trick kwenye ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Everton katika mechi Emirates, Februari 2018 wakati huo Arsenal ilikuwa chini ya Arsene Wenger.

 

Bournemouth - Wilson vs Huddersfield (2017)

Straika, Callum Wilson ndiye mchezaji wa mwisho kuifungia hat-trick Bournemouth na hiyo ilikuwa mwaka 2017. Katika mechi hiyo, Wilson aliweka kwenye nyavu mara tatu wakati alipoisaidia Bournemouth ilipoikandamiza Huddersfield 4-0, Novemba 2017. Tangu wakati huo, hakuna mchezaji mwingine kwenye kikosi hicho aliyetupia nyavuni mara tatu kwenye kikosi hicho ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja umeshapita sasa.

 

Brighton - Smith vs Coventry (1980)

Mchezaji wa mwisho kufunga mara tatu katika mechi moja ya ligi kwa kikosi cha Brighton alikuwa Gordon Smith na hiyo ilitokea karibu miaka 40 iliyopita. Staa huyo wa Scotland alisajiliwa na Brighton kwa ada iliyoweka rekodi wakati huo, Pauni 35,000 kutoka Rangers na alionyesha thamani yake kwa kufunga hat-trick kwenye mechi dhidi ya Coventry, Oktoba 1980.

 

Burnley - Gray vs Sunderland (2016)

Andre Gray ni mchezaji wa mwisho kwenye kikosi cha Claret kuondoka nyumbani na mpira uliochezewa kwenye mechi. Fowadi huyo ambaye kwa sasa anayekipiga kwenye kikosi cha Watford alifunga hat-trick kwenye mechi ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Sunderland, Desemba 2016.

Kwa maana hiyo, kwenye kikosi cha Burnley kwa sasa hakuna mchezaji aliyewahi kuifungia timu hiyo mabao matatu kwenye mechi moja.

 

Chelsea - Hazard vs Cardiff City (2018)

Si kitu kinachoshangaza kwamba kuona mchezaji wa mwisho wa Chelsea kufunga hat-trick kwenye mechi ya ligi ni supastaa wao, Eden Hazard. Mkali huyo wa Kibelgiji akiwa kwenye uzi wa The Blues aliweka mpira kwenye kamba mara tatu katika mechi moja. Hazard alipiga tatu kwenye mechi dhidi ya Cardiff City, Septemba 2018, wakati Chelsea walipoibuka na ushindi wa mabao 4-1 uwanjani Stamford Bridge.

 

Crystal Palace - Bolasie vs Sunderland (2015)

Yannick Bolasie alikuwa mchezaji wa mwisho kuwafungia Crystal Palace hat-trick kwenye mechi za ligi. Staa huyo alifanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Sunderland, wakati Palace waliposhinda 4-1, Aprili 2015. Winga huyo wa Congo amerejea kwenye kikosi cha Everton baada ya kusitisha mkataba wake wa mkopo huko Aston Villa kwenye Championship.

 

Everton -  Rooney vs West Ham (2017)

Kinara namba mbili wa mabao kwenye Ligi Kuu England, Wayne Rooney ni mchezaji wa mwisho kuifungia hat-trick Everton kwenye ligi. Straika huyo veterani alifunga mara tatu kwenye mechi moja ya ligi wakati Everton walipoichapa West Ham United 4-0 msimu uliopita. Kwenye mabao hayo, aliyofunga Novemba 2017, lilikuwa bao bora kabisa la msimu.

 

Fulham - Pogrebnyak vs Wolves (2012)

Fulham wanapambana kwa nguvu zote kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Kwenye historia ya timu hiyo, mchezaji wa mwisho kuwafungia hat-trick kwenye ligi alikuwa Pavel Pogrebnyak na alifanya hivyo Machi 2012.

Straika huyo raia wa Russia alifanya mambo yake hayo matata kabisa uwanjani na kuondoka na mpira nyumbani ilikuwa kwenye mechi dhidi ya Wolves, ambapo Fulham walishinda 5-0.

 

Leicester City - Vardy vs Man City (2016)

Hapa hakuna anayeshangaa kuona jina la Jamie Vardy kuwa ndiye mchezaji wa mwisho kuifungia hat-trick kwenye ligi. Vardy alitakatisha Leicester City kwenye mechi ya ligi Desemba 2016, wakati alipofunga mara tatu mbele ya timu ngumu kabisa, Manchester City. Mechi hiyo iliyofanyika uwanjani King Power, Vardy alipiga tatu Leicester ikishinda 4-2.

 

Liverpool - Firmino vs Arsenal (2018)

Kwenye kikosi cha Liverpool, mchezaji wao wa mwisho kufunga hat-trick alikuwa Mbrazili, Roberto Firmino na amefanya hivyo ndani ya msimu huu unaoendelea kwa sasa. Firmino alitupia tatu kwenye mechi ya ushindi wa mabao 5-1 mwezi uliopita wakati walipoifanya vibaya Arsenal uwanjani Anfield. Hiyo ilikuwa hat-trick ya pili kwa mwezi Desemba kwa kikosi cha Liverpool baada ya Mohamed Salah kutangulia kufunga wiki kadhaa nyuma.

 

Man City - Aguero vs Huddersfield (2018)

Straika, Sergio Aguero ndiye mchezaji wa mwisho wa Manchester City kuwafungia hat-trick kwenye ligi, wakati staa huyo alipofanya hivyo Agosti 2018. Kwa Aguero hiyo ilikuwa hat-trick yake ya tisa, wakati alipoweka kwenye kamba mipira mara tatu kuiongoza Man City ya kocha Pep Guardiola kutoa kipigo kizito kwa Huddersfield cha mabao 6-1 uwanjani Etihad.

 

Man United - Van Persie vs Aston Villa (2013)

Kwenye kikosi cha Manchester United, licha ya kuwa na washambuliaji wake wa maana kabisa akiwamo Romelu Lukaku, lakini mchezaji wao wa mwisho kufunga hat-trick kwenye ligi ni Mdachi Robin van Persie, wakati alipofanya hivyo Aprili 2013, Man United walipoichapa Aston Villa 3-0. Van Persie alifunga mabao yote kwenye mechi hiyo na hakika kiwango chake bora cha kutupia mipira wavuni kilimpa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu kwa msimu huo uliokuwa wa mwisho wa Man United kubeba ubingwa wa England.

 

Newcastle - Wijnaldum vs Norwich (2015)

Ni zaidi ya miaka mitatu sasa tangu Newcastle United kwa mara ya mwisho iliposhuhudia mchezaji wake akifunga hat-trick kwenye mechi ya Ligi Kuu England. Georginio Wijanldum, ambaye kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Liverpool, ndiye mchezaji wa mwisho kuifungia Newcastle mabao matatu kwenye mechi moja ya ligi wakati alipoisaidia timu hiyo kuichapa Norwich City 6-2 uwanjani St James’ Park, Oktoba 2015. Wakati sasa wababe hao wanaonolewa na Rafa Benitez wakitambana na hali yao, Mdachi huyo bado anashikilia rekodi yake huko kwenye kikosi hicho.

 

Southampton - Mane vs Man City (2015)

Staa mwingine wa sasa wa Liverpool, Sadio Mane anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa mwisho kufunga hat-trick kwenye Ligi Kuu England huko kwenye kikosi cha Southampton. Fowadi huyo Msenegali aliweka wavuni mara tatu katika mechi moja wakati Southampton walipojipigia Manchester City 4-2 katika mchezo mkali kabisa wa ligi uliofanyika Mei 2015. Kwa sasa Mane anafanya yake huko Anfield akiisaidia timu hiyo kuongoza ligi msimu huu kwenye mchakamchaka wao wa kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England.

 

Tottenham - Kane vs Southampton (2017)

Straika, Harry Kane ndio mchezaji wa mwisho kuifungia hat-trick Tottenham Hotspur kwenye Ligi Kuu England wakati alipoisaidia timu yake kuichapa Southampton 5-2 Desemba 2017. Lakini, mabao hayo matatu aliyofunga kwenye mechi moja ya ligi ni muda mrefu umeshapita kwa sababu ni mpaka sasa na fowadi huyo matata kabisa Mwingereza hajaifungia Spurs bao tatu kwenye mechi moja ya ligi. Kwa sasa Kane ni majeruhi na anatazamiwa kurudi uwanjani mwezi Machi.

 

Timu nyingine

Kwenye kikosi cha Watford, mchezaji wao wa mwisho kufunga hat-trick kwenye ligi alikuwa, Mark Falco na hiyo ilikuwa miaka 35 iliyopita huko, wakati alipofunga tatu kwenye mechi dhidi ya Aston Villa iliyofanyika Oktoba 1986. West Ham United wao rekodi zao zinaonyesha kwamba mchezaji wao wa mwisho kuwafungia hat-trick kwenye ligi alikuwa Andy Carroll, ambaye alifanya hivyo kwenye mechi ya sare ya 3-3 dhidi ya Arsenal, Aprili 2016. Wolves ndio kama hivyo, Jota ndio mchezaji wao wa mwisho, wakati kwa timu kama Cardiff City yenyewe haina mchezaji yeyote aliyewahi kufunga hat-trick kwenye ligi sawa na ilivyo kwa Huddersfield.