Wachezaji wa Zanzibar hoi washindwa kufanya mazoezi

Muktasari:

Zanzibar inashika mkia katika Kundi A ikiwa imefungwa mabao 10 katika mechi zake mbili za awali dhidi ya Sudan Kusini na Burundi na kupoteza nafasi ya kusonga mbele kwa mashindano hayo.

Dar es Salaam.Hali si shwari katika kambi ya timu ya soka ya Taifa ya Wanawake ya Zanzibar leo imeshindwa kufanya mazoezi na taarifa zinadai huenda wasicheze mechi ya kesho dhidi ya Tanzania Bara.

Zanzibar inashika mkia katika Kundi A ikiwa imefungwa mabao 10 katika mechi zake mbili za awali dhidi ya Sudan Kusini na Burundi na kupoteza nafasi ya kusonga mbele kwa mashindano hayo.

Leo asubuhi timu hiyo ilikuwa na ratiba ya kufanya mazoezi, lakini ikatokea hali ya sintofahamu wachezaji 14 wakadaiwa kuwa na maumivu.

Pia, inaelezwa morali ya wachezaji hakuna tena na kuna wanaoshauri, timu isiingie uwanjani kukipiga mchezo wa kesho wa kukamilisha ratiba na Tanzania Bara.

Akizungumzia suala hilo Kocha Mohammed Salah alisema aliamua kuwapumzisha wachezaji kwa sababu zaidi ya wachezaji wake 10, wana maumivu.

"Kweli leo tumepumzika kama nilivyokwambiwa wachezaji wanaumwa, lakini kesho asubuhi kabla ya kucheza mechi yetu jioni tutanyoosha misuli,"alisema Salah.

Kuhusu kutoingiza timu uwanjani katika mchezo wa kesho kocha Salah alisema sijui jambo hilo, sisi tunaendelea vizuri kama kawaida, kesho tutaingiza timu uwanjani kama kawaida.

Awali, Salah alisema kikosi chao kinataka kufanya vizuri kwenye mechi yao ya mwisho na Tanzania Bara na alisema, hawaogopi.

"Tunajua Tanzania Bara wazuri, lakini pamoja na yote wasije wakijiaminisha watachukua ushindi kirahisi," alisema Salah.