Wachezaji hawa wamebamba kinoma AFCON

Muktasari:

Pazia la Mashindano ya AFCON mwaka huu litafungwa rasmi Ijumaa, Julai 19 katika mchezo wa Fainali utakaozikutanisha Senegal na Algeria ambao utachezwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.

Dar es Salaam. Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu huku Misri zinaelekeag ukingoni ambapo sasa kunangojewa mechi mbili za kuhitimisha mashindano hayo.

Mechi hizo mbili ni ile ya kusaka mshindi wa tatu ambayo itazikutanisha Tunisia na Nigeria pamoja na ule wa Fainali ambao utakuwa baina ya timu za Algeria na Senegal.

Wakati mashindano hayo yakielekea ukiongoni, wapo watu ambao hadi wameonekana kufanya vyema na kutamba katika maeneo tofautitofauti ya mashindano hayo ambao wanaweza kuwa marefa, wachezaji, mashabiki ama timu.

Makala hii inakupa dondoo za watu ambao hadi mashindano hayo yanakaribia kufika tamati, wametamba au kung'aa kwa namna moja au nyingine.

Mustapha Ghorbal & Bamlak Tessema Weyesa

Refa Mustapha Ghorbal kutoka Algeria na mwenzake Bamlak Tessema Weyesa wa Ethiopia ndio waamuzi wa kati waliochezesha idadi kubwa ya mechi kwenye Fainali za AFCON mwaka huu ambapo kila mmoja ameshika kipyenga kwenye mechi nne.

Ghorbal amechezesha mechi baina ya Mechi alizochezesha ni kati ya Zimbabwe na DR Congo, Ivory Coast dhidi ya Afrika Kusini, Uganda dhidi ya Senegal na ile ya Senegal dhidi ya Benin.

Naye Tessema amechezesha mechi baina ya Senegal na Tunisia, Tunisia na Angola, Ghana na Cameroon pamoja na ile ya  Algeria na Ivory Coast.

Odion Ighalo (Nigeria)

Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Nigeria, ndiye kinara wa kupachika mabao kwenye AFCON hadi sasa ambapo amefumania nyavu mara nne katika mechi ambazo Nigeria ilicheza dhidi ya Algeria, Burundi na Cameroon.

Nyuma ya Ighalo kuna Sadio Mane (Senegal), Adam Ounas na Ryad Mahrez(Algeria) na Cédric Bakambu (DR Congo) ambao kila mmoja amepachika mabao matatu.

Franck Kessié (Ivory Coast)

Ivory Coast imeaga mashindano baada ya kutolewa na Algeria kwenye hatua ya robo fainali lakini kiungo wake Franck Kessié ndiye kinara wa kupiga pasi za mwisho akiwa amefanya hivyo mara tatu.

 

Wanaomfuatia Kessié ni Islam Slimani na Ismael Bennacer wa Algeria, Moussa Doumbia (Mali), Abdul Rahman Baba (Ghana), Moses Simon (Nigeria), Farouk Miya (Uganda), Lamine Gassama (Senegal), Ayman Ashraf (Misri) na Cebio Soukou (Benin) ambao kila mmoja a,epiga pasi mbili zilizozaa mabao.

 

Wahbi Khazri (Tunisia)

Nyota huyo wa Tunisia anaongoza kwa kutengeneza idadi kubwa ya nafasi kwenye fainali za AFCON kuliko mchezaji mwingine yeyote hadi sasa akiwa amefanya hivyo mara 16.

Youcef Belaïli wa Algeria anashika nafasi ya pili akiwa ametengeneza nafasi 12 huku Adama Traoré II yeye akishika nafasi ya tatu kutokana na nafasi 11 alizotengeneza.

Yassine Meriah (Tunisia)

Katika mechi sita alizoichezea Tunisia, Yassie Meria ndiye mchezaji aliyepiga pasi idadi kubwa ya pasi hadi sasa ambazo ni 377 akifuatiwa na Ellyes Skhiri aliyepiga pasi 322 na nyota mwingine wa nchi hiyo Dylan Bronn anashika nafasin ya tatu akiwa amepiga pasi 305.

Mohamed El-Shenawy (Misri)

Kipa Mohamed El-Shenawy wa Misri ndiye ameongoza kwa kuokoa michomo mingi kwenye fainali za AFCON mwaka huu ambapo hadi sasa ameokoa jumla ya mashambulizi 15.

Shenawy anafuatiwa kwa ukaribu na Llyod Kazapua wa Namibia aliyeokoa mashambulizi 15 na Mouez Hassen ambaye naye kaokoa mashambulizi 15 na nafasi ya nne inashikiliwa na Aishi Manula wa Tanzania aliyezuia michomo 14.

Alfred Gomis & Rais M'bolhi

Makipa Alfred Gomis wa Senegal na Rais M'bolhi wa Algeria ndio vinara wa kutoruhusu nyavu zao kutikiswa katika idadi kubwa ya mechi ambapo kila mmoja amecheza jumla ya mechi nne bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa.