Wachezaji Ndanda FC wazuiwa hotelini Singida

Muktasari:

Ligi Kuu Bara msimu huu inachezwa bila ya kuwa na mdhamini mkuu baada ya kampuni ya Vodacom kujitoa

Dar es Salaam. Jinamizi la kukosa udhamini wa Ligi Kuu Bara limeanza kuonekana baada ya wachezaji wa Ndanda FC kuzuiwa kuondoka katika Hotel ya City Garden mjini Singida kwa kushindwa kulipa Sh 3milioni.

Ndanda ilikuwa mkoani Singida kucheza mechi ya Ligi Kuu mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Singida United na kuambulia kipigo cha mabao 3-0.

Afisa Habari wa Ndanda Fc, Idrisa Bandali, amesema timu hiyo imeshindwa kuondoka Singida kurejea Mtwara baada ya kukosa fedha kwa ajili ya usafiri huku pia wakidaiwa zaidi ya Sh. 3Milioni za chakula na ,alazi.

Katibu wa timu hiyo Seleman Kachele aliliambia Mwanaspoti Online kwamba timu hiyo bado ipo Singida na viongozi wanaendelea na mchakato wa kupata fedha za kulipa deni hilo.

"Kama tutapata fedha hizo jioni ya leo basi tutawalipa na timu itaondoka kurejea Mtwara kwa ajili ya maandalizi mengine, kiukweli hali ni mbaya.

"Nitumie nafasi hii kuwaomba wadau wa timu ya Mtwara kutuunga mkono hususani kipindi ambacho ligi haina mdhamini, tunahitaji kuwa washindani, lakini tukikosa fedha za mahitaji muhimu kwa timu mwisho wa picha itakuaje,"alisema.

Alipoulizwa kocha mkuu wa timu hiyo, Malale Hamsini amesema anaendelea na programu yake ya mazoezi na kudai hayo mambo ya timu kuondoka ama kutoondoka ni jukumu la mabosi wake.

"Kazi yangu ni kufundisha na timu imefanya mazoezi kwa muda wote amabo tumekaa Singida, kama tumebaki kwa ajili ya kukosa pesa mimi sijui tukitakiwa kuondoka tutafanya hivyo," anasema Malale.