Wachambuzi wazungumzia Kundi la Harambee Stars

Muktasari:

  • Oliech aliyeipeleka Stars AFCON 2004 kwa kupachika bao la kipekee kwenye mechi ya mwisho iliyokuwa lazima washinde, dhidi ya Cape Verde akiifuma kunako dakika ya 83.

BAADA ya droo ya dimba la AFCON 2019 kufanywa siku chache zilizopita na  Harambee Stars kupangwa kwenye kundi gumu C inayojumulisha vile vile Tanzania, Senegal na Algeria, wachanganuzi kibao nje na ndani ya nchi wametoa maoni yao.

Mdau wa hivi karibuni kuongezea kauli yake ni straika mkongwe Dennis ‘The Menace’ Oliech. Oliech ambaye aliunda kikosi cha mwisho cha Stars kilichoshiriki AFCON miaka 15 iliyopita kabla ya sasa, katoa darasa la ni kipi kinachopaswa kufanyika pale Stars ili kuwa na matumaini ya kufuzu angalau kutoka kundini.

Oliech aliyeipeleka Stars AFCON 2004 kwa kupachika bao la kipekee kwenye mechi ya mwisho iliyokuwa lazima washinde, dhidi ya Cape Verde akiifuma kunako dakika ya 83, kazungumizia mambo kadhaa wa kadha wanaotakiwa kufanya sio tu wachezaji bali pia makocha na uongozi.

Tusipoteze mechi ya ufunguzi

Kulingana na Oliech ambaye toka arejee kwenye soka akitokea kustaafu, ameishia kuibua mdahalo mkubwa kuhusu uwezekano way eye kurejeshwa kwenye timu ya  taifa, kasisitiza kuwa ni vyema Stars kuhakikisha hawapotezi mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Algeria. Mechi hiyo itachezwa Juni 30 na siku nne baadaye wapambane na Tanzania.

Mtazamo wa Oliech ni kwamba, kupoteza mechi hiyo ya kwanza kutavuruga morali ya Stars na huenda wakashindwa kung’aa kwa itakayofuatia.

“Wafanye lolote lile lipo kwenye uwezo wao kuhakikisha kwamba hatupotezi mechi ya kwanza. Tukipoteza mechi hiyo, timu itajisababishia presha kubwa kuelekea mechi zijazo jambo ambalo linaweza kuwasukuma kufanya makosa kwenye michuano hiyo itakayofuatia na tuishie kufedheheshwa hata zaidi. Hili ni muhimu sana kuzingatia” Oliech alisema.

Oliech anasisitiza kuwa hata sare kwenye mechi ya kwanza itatosha. Lakini itakuwa bora zaidi kama Stars wakiangukia ushindi kwa sababu hiyo itaisaidia timu kutulia.

Migne asiwe mwepesi na panga pangua

Kingine alichoshauri Oliech ni kumsihi kocha Mfaransa Sebastina Migne kujiepusha na panga pangua ya kikosi na badala yake kusalia na ile timu aliyotumia kwenye mechi za kufuzu kwa hatua ya  makundi.

“Kocha asifanye mabadiliko japo kama ni lazima, kwenye timu aliyoitumia kufika hapa, kwa sababu tayari wameshasomana mchezo na kila mmoja anamwelewa mwenzake. Kama akifanya hivyo hili litaleta ushikamano na ushirikiano mwema kwenye timu. Mabadiliko mengi yanaweza kuvuruga ushikamano na ushirikiano huo na hapo makosa yatatokea.” Akaongeza.

Wachezaji wasitishike.

Kwa wengi wa wachezaji timuni, ni wachache mno kama wapo, waliowahi kupata fursa ya kucheza soka katika kiwango hichi cha kimataifa. 

Oliech anafahamu bayana kuwa kwenye levo kama hii, ni kawaida kwa wachezaji ambao hawajazoea kushikwa na hofu kutokana na ule munkari utakaokuwa uwanjani ambao huwa sio wa kawaida.

“Wachezaji watakaochaguli wajitahidi kutotafunwa na uwoga kutokana na ukubwa wa ngoma hii. Hizi ni mechi kama tu zingine hivyo wajitahidi sana kuingia katika kila mechi wakiwa wametulia”

Mastraika wasituangushe

Kikubwa zaidi kwa utathamini wa Oliech ni mshango utakaotolewa na washambuliaji, wakiongozwa na chaguo la kwanza Miachel Olunga mabaye kocha Migne kaweka wazi kuwa ndiye mchezaji wa pekee mwenye uhakika wa kupata namba kwenye kikosi chake cha kwanza.

“Kwa mashindano kama haya, mpango mzima huwa ni magoli mnayofunga. Haijalishi mtindo au staili mtakayocheza iwe ya kuvutia au ya kuboa hapa mpango mzima ni magoli tu. Hivyo mastraika wetu wanahitaji kuwa makini sana kwa kuwa fursa watakazopata, wasisipopoteze. Sio kawaida kwa mashindano kama haya kuwa na fursa nyingi za kufunga” Oliech alizidi.

Zipangwe mechi za kirafiki

Oliech anasema ni kwa mpango kama huu ndio timu itaweza kujifua hata zaidi na kujiweka kwenye mazingara ya kiushindani.

“Baada ya kufuzu 2004, hatukushiriki  mechi za kutosha za kirafiki ili kupima kiwango cha matayarisho yetu na tuliishia kupoteza mechi zote. Uongozi wa kipindi kile haukujali angalau huu wa sasa umefanya mawili matatu na naamini kama tukipata mechi za kirafiki, raundi hii mambo yatakuwa tofauti kidogo”