Wababe wa Simba wamtisha Minziro!

Friday January 11 2019

 

By SADDAM SADICK

USHINDI walioupata Mashujaa FC ugenini dhidi ya Trans Camp umempa jeuri kocha wake, Atugo Manyundo ambaye ametamba kuwa kwa sasa akili yake inafikiria mechi na Arusha United kuhakikisha wanafanya kweli katika mchezo huo.

Timu hiyo imekuwa mwiba baada ya kuweka historia ya kuiondoa Simba kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho kwa mabao 3-2 na sasa inatesa katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Manyundo alisema kwa sasa hawataki masihara kwani malengo yao ni kupanda Ligi Kuu msimu ujao, hivyo mechi yao na Arusha United inayonolewa na Fred Felix ‘Minziro’ itakayopigwa kesho Jumamosi katika Dimba la Lake Tanganyika, Kigoma anahitaji ushindi tu.

Alisema kikosi chake kwa sasa kina ari nzuri na kwamba atawaandaa kisaikolojia wachezaji wake kuhakikisha wanashuka uwanjani kutafuta alama tatu ili kujiweka nafasi nzuri.

“Malengo yetu ni kupanda Ligi Kuu, hivyo lazima kila mchezo kwetu uwe fainali, tunataka ushindi mechi ya Jumamosi dhidi ya Arusha United, nitawaandaa vijana wangu kisaikolojia,” alisema.

Advertisement