Waarabu wamtaka Mukoko, Yanga ikizubaa imeumia

Monday September 14 2020

 

By MWANDISHI WETU

YANGA imeshuka uwanjani usiku wa jana kwenye mchezo wao wa pili wa Ligi kuu Bara dhidi ya Mbeya City, huku kiungo wao fundi Mukoko Tonombe akiwaponyoka Waarabu waliokuwa wakimwinda kabla ya kujiunga na chama la Jangwani.

Aidha ufundi alioonyesha kiungo huyo kwenye mechi chache alizoichezea Yanga, imeelezwa ni hazina ambayo mabosi wa Jangwani wanapaswa kuilinda la sivyo anaweza kuwatoka kwani anaonekana ni mchezaji mwenye kiwango cha kimataifa zaidi.

Tuanze na ishu yake na Waarabu. Inaelezwa, kiungo huyo aliyekuwa AS Vita amepishana na fuko la fedha baada ya klabu moja ya Saudi Arabia kumkosa kumnyakua akiwa tayari Yanga imeshamalizana naye na kumleta jijini Dar es Salaam.

Iko hivi, meneja wa mchezaji huyo Nestor Mutuale amefichua Klabu ya Al Nassr ya Saudia ilitua DR Congo ili kumuulizia Tonombe kwa nia ya kutaka kununua mkataba wake.

Mutuale ameliambia Mwanaspoti, Al Nassr ilikuwa inajua kiungo huyo ametolewa kwa mkopo kuja Yanga na kutaka kuununua mkataba wake wakiweka mezani kiasi cha dola 100,000 (kiasi cha Sh 230 milioni za Kitanzania).

“Hii ni mara ya pili wanakuja kumtaka Mukoko lakini mara ya kwanza walikuja wakati ugonjwa wa Covid 19 umechangamka wakasema watarudi lakini sasa wamechelewa,” alisema Mutuale.

Advertisement

Kiasi hicho cha fedha ambacho Al Nassr walikitenga kwa Tonombe ndio kiasi ambacho matajiri wa Yanga GSM walikitumia kuwasajili kiungo huyo na winga Tuisila Kisinda mapema mwezi uliopita, Yanga ikinunua mikataba yao ndani ya AS Vita na Union Maniema.

Yanga ikiwasainisha mikataba ya miaka miwili kila mmoja ambayo itafikia tamati Julai 2022.

Mutuale alisema kama Yanga ingechelewa kidogo kumsajili Tonombe, Vita isingekubali kuwauzia kiungo huyo na wangekimbilia haraka kufanya biashara na Al Nassr.

“Vita sasa inaangalia sana fedha sidhani kama wangekubali kuwauzia Yanga kama hawa Al Nassr wangefika mapema Yanga ni kama bahati kwao.”

Naye Meneja wa Vita, Diba Ilunga amethibitisha taarifa hizo akisema tayari walishawapa majibu Al Nassr wakiwaambia Tonombe sasa ni mali ya Yanga na wawasiliane na mabosi wa klabu hiyo. Ilunga alisema kwasasa kikosi chao kipo katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya huku kocha wao Florent Ibenge akiendelea na kazi ya kutafuta mrithi ya Tonombe na mmoja wa wanaojaribiwa ni nahodha wa zamani wa Yanga Papy Tshishimbi

“Nikweli walikuja hao (Al Nassr) walichelewa wenyewe, hawakutaka kumaliza mambo haraka, walipokuja Yanga Rais wa klabu akafanya biashara,” alisema Ilunga na kuongeza;

“Timu yetu sasa ipo kambini nje kidogo ya Kinshansa kocha wetu anaendelea kutengeneza timu wapo pia wachezaji wanaangaliwa kama tutaona wanaweza kutusaidia yupo yule alikuwa Yanga Kabamba (Tshishimbi), kocha ndio ataamua.”

MSIKIE KASHASHA

Hakuna kiongozi wa Yanga aliyepatikana kueleza kama watakuwa radhi kumuachia kiungo huyo kama waarabu watawafuata ili wambebe, kwani simu zao zilikuwa zikiita bila majibu, lakini Mchambuzi maarufu wa soka nchini, Alex Kashasha amemchambua Tonombe na kudai Yanga imepata jembe na lazima walichunge ili asiwatoroke.

Kashasha alisema kwa mechi chache alizomuona ni mchezaji ambaye ni fundi kwenye kiungo cha ukabaji akiwa na uwezo wa kumiliki mpira na mwenye jicho la kupiga pasi hatarishi sambamba na kujiamini akiwa na umbo linalombeba.

“Hata kama ni ngumu kumpima kwa sasa, kwani amejiunga na timu ambayo hajazoeana na wenzake, lakini kiufundi jamaa ni fundi kwelikweli kwani ana ‘first touch’, yupo makini ana nguvu na urefu wake unamsaidia lakini anajiamini sana na anajua anachokifanya uwanjani,” alisema Mwalimu Kashasha na kuongeza;

“Kwa sasa inamsumbua, kwa vile ni mara ya kwanza kucheza soka Tanzania, ni lazima asome utamaduni wa Yanga, ila akiizoea atasumbua na niseme tu, Yanga imepata jembe la maana lazima wamuangalie kwani anajua anachokifanya uwanjani.”

Kashasha alisema kutaka kujua Tonombe ni balaa akizoeana na wachezaji wenzake ni aina ya pasi alizokuwa akipiga kwa Kisinda anayemjulia tangu akicheza naye As Vita, huku akisisitiza jamaa ni moja ya viungo bora Afrika.

 

Advertisement