TIMUA VUMBI : Waamuzi TPL mjipange kweli kweli kuna vita huko

Muktasari:

Waamuzi watakuwa na kazi ngumu pengine hata kubeba lawama kuwa maamuzi yao sio sahihi lakini kubwa mabadiliko ya baadhi ya sheria ndiyo yatakayosababisha waonekane maamuzi yao si sahihi. Hivyo tunatarajia kutokea hayo katika mpira.

Wikiendi Ligi Kuu Bara inaanza rasmi iki ni msimu mpya kabisa wa 2019/20 na timu 20 zinawania taji linaloshikiliwa na Simba.
Simba wanashikilia ubingwa wa TPL kwa mara ya pili mfululizo na wamejipanga kupigana vita ili watwae ubingwa huo mara tatu mfululizo kama ilivyowahi kuwa kwa watani zao Yanga kabla hawajavuliwa ubingwa huo.
Kila timu imesajili, imefanya maandalizi ya kutosha kuelekea msimu huo mpya na hakuna timu inayitarajia kufanya vibaya hivyo ushindani utakuwa ni mkubwa na pengine hata kwenye kuamua uwanjani kutakuwa kugumu.
Hata hivyo, yote kwa yote dakika 90 zitaamua nani mbabe wa mechi hiyo ambayo inakuwa chini ya waamuzi wanne ama sita kwasasa ili kuongeza umakini zaidi.
Baadhi ya sheria za soka zimebadilika ama kuboreshwa zaidi hivyo huenda kutakuwa na vitu vigeni ambavyo baadhi yao hawatevielewa na hii ni kuanzia kwa wachezaji, makocha na mashabiki wao.
Waamuzi watakuwa na kazi ngumu pengine hata kubeba lawama kuwa maamuzi yao sio sahihi lakini kubwa mabadiliko ya baadhi ya sheria ndiyo yatakayosababisha waonekane maamuzi yao si sahihi. Hivyo tunatarajia kutokea hayo katika mpira.
Ingependeza zaidi kabla ya ligi kuanza yatolewe mafunzo juu sheria za soka hasa ambazo zina mabadiliko ama kuboreshwa mafunzo hayo yaanzie kwa wachezaji wenyewe pengine nao hawaelewi na wanaweza kuleta ubishani uwanjani pale ambapo mwamuzi anatoa maamuzi yake.
Mafunzo ya muda mfupi yanasaidia sana kutoa mwanga kwa wachezaji na makocha wao maana kwa hakika sio wachezajj wote wanaoelewa sheria zote 17 za soka kiundani zaidi, wataonekana wameonewa na hawatendewi haki kwenye mpira wao ambao ndio ajira yao.
Pia waamuzi msitumie kigezo hivho cha watu kutokuwa na uelewa mzuri juu ya sheria hizo, mnapaswa kuwa weledi kwenye kazi zenu pasipo kuangalia hii ni timu gani inacheza, iwe timu kongwe ama changa kwenye ligi.
Weledi wenu ndiyo husaidia soka la Tanzania kuw ana heshima ikiwemo kukuwa kwenye viwango bora vya juu kimataifa lakini pale mnapoharibu mpira kila kitu kinakwenda vibaya ikiwa na maana mpira hauwezi kusonga mbele maana lengo la kuchezesha kwa kuvunja sheria ni kushusha mpira huu.
Achalia mbali na hilo, mwamuzi anapokuwa makini na kazi yake basi atakubalika ndani na nje ya nchi kwa kupata nafasi za kuchezesha michezo mikubwa ya kimataifa kwani hatakuwa na skendo mbaya za kuvunja sheria makusidi kwa kuipendelea timu fulani ishinde ama ipate matokeo mazuri.
Wakati timu zinapaga kuwania ubingwa basi waamuzi pambaneni kulinda heshima zenu za kazi kwa kutenda yaliyosahihi uwanjani pasipo kuvunja sheria na kutoogopa ukubwa ama udogo wa timu.
Heshima ya waamuzi inatengenezwa na waamuzi wenyewe, pia kushushwa heshima yao nako kunatengenezwa na wao wenyewe kwa kuvunja na kutofuata sheria na kanuni za kazi zao, huku wakiangalia masilahi yao binafsi.
Wanasema soka ni mchezo wa wazi, kila mtu anaona kinachoendelea uwanjani, hivyo uwazi huo ndiyo unaoonyesha ubora wa kazi yenu kwa jamiii, unawapa sifa nzuri na mbaya kwa kutegemea na nini kimefanywa na nyie.
Ni kazi ngumu kumridhisha kila mmoja ila kwa kuwa mweledi basi ni kazi rahisi sana maana mwamuzi ataongozwa na sheria, kanuni za soka huku utu na busara ukiwa wa mwisho ambao nao ni muhimu sana kwenye michezo kwani wote wanaocheza ni binadamu.
Tunatarajia msimu huu lawama hazitakuwepo ingawa si kazi rahisi kuzikwepa, ila hata zikiwepo zisiwe zile za makusudi mpaka mwamuzi ifikie hatua analindwa na askari ili atoke uwanjani kisa tu ameamsha hasira za watu kwa kuchezeaha vibaya.
Waamuzi msimu ujao mna kazi kubwa ya kulinda heshima zenu kwenye soka lakini pia wachezaji na makocha kwa siku zilizobaki pitieni tena sheria na kanuni za soka ili kujikimbusha baadhi ya mambo. Kila la kheri kwa kila timu.