Waamuzi Simba, Yanga wakiri walishangilia. Wafunguka sababu

Muktasari:

Waamuzi watano kati ya sita waliochezesha mechi hiyo ya nusu fainali ya kombe la Shirikisho (FA) ambayo Simba ilishinda mabao 4-1 walipiga picha wakifurahi wakiwa vyumbani.

WAKATI picha ya waamuzi wa mechi ya Simba na Yanga (pichani) wakionekana wakishangilia wakiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ikiibua mjadala, wenyewe wameanika ukweli.

Waamuzi watano kati ya sita waliochezesha mechi hiyo ya nusu fainali ya kombe la Shirikisho (FA) ambayo Simba ilishinda mabao 4-1 walipiga picha wakifurahi wakiwa vyumbani.

Picha ambayo iliibua mjadala huku baadhi wakichangia kwa kuandika waamuzi walisherehekea baada ya timu yao ya Simba kushinda mabao 4-1, hata hivyo uongozi wao umefafanua tuhuma hizo.

Picha ambayo waamuzi hao wamekiri walipiga siku ya mechi hiyo, lakini wamesisitiza walipiga kwa ajili ya kuondoa tensheni ya mchezo.

“Ni kweli siku ya mechi ya Simba na Yanga nilikuwa na waamuzi waliochezesha mechi hiyo ambao walikuwa wakiimba na kucheza,” alisema Makamu Mwenyekiti wa kamati ya waamuzi, Israel Nkongo.

Waamuzi waliochezesha mechi hiyo ni Ramadhani Kayoko(aliyesimama kati),Aboubakary Mturo, Abdallah Mwinyi Mkuu, Nadeem Aloyce, Frank Komba, Kassim Mpanga huku kamisaa akiwa Ally Katolila.

Nkongo ambaye kabla ya mechi alipasha pamoja na waamuzi hao uwanjani, alisema walifanya hivyo ili kuondoa tensheni ya mchezo huo.

“Hiyo ni kawaida kwa waamuzi, nilikuja nao kwenye basi wakiimba na kucheza wakishangilia na hata tulipokuwa vyumbani, walifanya hivyo, wale pia ni binadamu. “Halafu mbona wachezaji wanapokuwa vyumbani huwa wanaimba na kucheza, kwa nini isiwe kwa waamuzi? Wanaosema waamuzi walikuwa wakisherehekea ushindi wa Simba si kweli, wameamua tu kuitumia picha hiyo vinginevyo,” alisema.

Alisema mpira ndivyo ulivyo, ingawa akashauri timu inapofungwa itafakari ilikosea wapi. “Binafsi sijaona sehemu ambayo waamuzi walitoa uamuzi wa upendeleo katika mechi ile,” alisema. Baada ya mchezo huo Yanga kupitia nahodha wao, Pappy Kabamba Tshishimbi na Kocha Luc Eymael walikiri kwamba timu hiyo ilizidiwa uwezo. Eymael alisema kuwa; “Kila mchezaji ajitafakari kwa kujiangalia kwenye kioo kile alichofanya kama bado anastahili kuendelea kuwepo.”

Katika mchezo huo, Yanga ilikubali kipigo hicho na kuondolewa katika harakati za kutafuta tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa kupitia ubingwa wa FA. Simba tayari imeshafuzu Ligi ya Mabingwa Afrika na Namungo itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika. Ligi Kuu inaendelea kwenye viwanja mbalimbali nchini leo ambapo Yanga itavaana na Singida United katika Uwanja wa Taifa Dar saa 1 usiku.