WASIKIE HAWA: Shabiki wa United hasira kama zote!

Muktasari:

Shabiki huyo anaamini klabu hiyo nafasi ya sita itawahusu tena msimu ujao.

MANCHESTER, ENGLAND.SHABIKI mmoja mwenye hasira wa klabu ya Manchester United ameamua kuichoma moto jezi yake aliyonunua ya timu hiyo na kisha kumsemea mbovu Ed Woodward kwa kuifanya timu hiyo kuwa kichekesho.
Shabiki huyo aliamua kuposti video kwenye Twitter inayomwonyesha akiichoma moto jezi ya ugenini ya Man United na kisha kusema maneno machafu kwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Woodward kwa kushindwa kufanya usajili wa maana hadi dirisha lilipofungwa.
Man United ilikuwa ikitajwa kuwa na mpango wa kuwasajili Bruno Fernandes, Paulo Dybala na Christian Eriksen, lakini hadi dirisha linafungwa juzi Alhamisi hakuna hata mmoja aliyetua huko Old Trafford, huku wao wakimuuza straika Romelu Lukaku kwenda Inter kwa ada ya Pauni 76.5 milioni na hakuna mtu wa kuziba pengo lake.

Shabiki huyo anaamini klabu hiyo nafasi ya sita itawahusu tena msimu ujao.
Aliandika: “Ndugu zangu Man United. Nimevunjika sana moyo kwa klabu yetu pendwa kufanywa kichekesho kwa ajili ya huyo mtu anayeitwa Woodward. Najaribu kuutazama msimu huu utakavyokuwa. Nafahamu wazi yatajirudia ya msimu uliopita #WoodwardOut.”
Kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya, Man United iliwasajili Daniel James, Aaron Wan-Bissaka na Harry Maguire.