WAMECHOMA: PENALTI ZILIVYOZIGHARIMU TIMU HIZI EPL

LONDON, ENGLAND. PENALTI ni tukio linalotokea mara chache sana uwanjani, lakini linaweza kusababisha mashabiki kukereka na wengine kufurahi.

Hukera kwa sababu ni rahisi sana kubadili ubao wa matokeo, na hufurahisha pia endapo ubao utabaki palepale, kwa maana ya wapigaji kukosa. Zipo timu katika Ligi Kuu England, linapotokea suala la penalti huwa hazibaahatishi, zinafunga na kuna nyingine zinaongoza kwa kusababisha penalti ambazo zinaishia kuwagharimu.

Hizi hapa timu tano za Ligi Kuu England msimu uliopita zilizosababisha penalti zilizowagharimu kupoteza michezo yao.

Tottenham (Penalti 5)

Katika mechi 38 za Ligi Kuu England msimu uliopita, Spurs iliruhusu mabao matano kutokana na penalti kati ya mabao 61 iliyofungwa.

Kati ya penalti hizo, beki wa kushoto wa timu ya Taifa ya Ivory Coast, Serge Aurier anaongoza kwa kusababisha penalti nyingi (2), huku msimu mzima ikiruhusu Jumla ya penalti saba.

Moja ya sababu inayotajwa kuiweka Spurs kwenye orodha hii ni mfumo anaotumia Kocha Jose Mourinho wa kuzuia na huchangia wachezaji kufanya faulo nyingi.

Bournemouth (Penalti 5)

Imeshuka daraja, lakini ni miongoni mwa timu zilizofanya faulo nyingi zilizozaa penalti. Kwa jumla ilizalisha penalti saba na kati ya hizo tano zilizalisha mabao.

Adam Smith alichangia penalti mbili, huku Steve Cook naye akichangia mbili kwa timu yao hiyo. Miamba hiyo ilimaliza ligi ikiwa ni timu ya tatu kwa kufungwa mabao mengi, ikifungwa jumla ya mabao 65.

Arsenal (Penalti 7)

Beki wa kati kutoka Brazil, David Luiz aliweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyesababisha penalti nyingi (5) kati ya nane na ilifungwa penalty saba.

Kutokana na mabao hayo, Arsenal ilijikuta ikipoteza pointi nyingi na kusababisha kumaliza nafasi ya nane mwisho wa msimu wa EPL.

Watford (Penalti 8)

Nayo imeshuka daraja. Hata hivyo, msimu uliopita moja ya yaliyochangia kuishusha ni kusababisha penalty nyingi zilizoigharimu.

Kwa jumla ilizalisha penati tisa na ikaruhusu nane kati ya hizo kutikisa nyavu zao. Golikipa Ben Foster alichangia zaidi kuzalisha penalti nyingi, pamoja na kiungo wake Will Hughes na kila mmoja alichangia mbili.

Mpaka msimu unamalizika ilifungwa jumla ya mabao 64 na kushika nafasi ya nne kwenye orodha ya timu zilizofungwa mabao mengi na kuaga rasmi EPL.

Leicester City (Penalti 11)

Ndio kinara wa kuzalisha penalti msimu uliopita. Licha ya kumaliza msimu ikiwa nafasi ya tano kwa alama 62, na wakati mwingine ilifika hadi top four na kusumbua timu pinzani, lakini ilisababisha penalti nyingi zilizowagharimu na kujikuta ikiondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa wa EPL.

Kwa jumla iliruhusu penalti 11 na kati ya hizo ilifungwa nane. Wilfred Ndidi ndiye aliyezalisha penalti nyingi (3), huku beki wa kati, Caglar Soyuncu alisababisha mbili.

Hata hivyo, licha ya kufanya makosa hayo, Leicester iliruhusu mabao 41 tu na kumaliza nafasi ya tano.