Vurugu Yanga zawatisha wagombea kuanza kampeni

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF, Ally Mchungahela

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF, Ally Mchungahela alisema kampeni zitaanza siku tano kabla ya uchaguzi ndivyo ilivyopangwa huku akiweka wazi sasa ni wakati wa rufaa na kupelekana kamati ya maadili.


KUELEKEA Uchaguzi wa Yanga wagombea waliopitishwa kuwania nafasi hizo wameingiwa na hofu kutokana na kupata vitisho kutoka kwa wanachama kitendo kilichosababisha kuomba zoezi la kampeni lisogezwe mbele.

Mmoja wa wagombea katika uchaguzi huo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema wameomba kampeni za uchaguzi huo zifanyike siku tano kabla ya uchaguzi kwa kuhofia vurugu kutokea kutokana na wanachama kugawanyika.

Alisema pamoja na wao kuchukua fomu lakini uchaguzi ni mgumu sana kwao kutokana na kupokea vitisho kutoka kwa wanachama ambao hawajapenda wao kuchukua fomu kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa madai kuwa ni wasaliti.

“Ndugu yangu si unaona uchaguzi wenyewe unavyoendeshwa ni ngumu sana kwetu kufanya kampeni za mapema sana kiasi hiki tunatarajia kuanza Januari 5 mwaka huu ikiwa ni siku tano kabla ya uchaguzi unaotarajia kuanza Januari 13,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF, Ally Mchungahela alisema kampeni zitaanza siku tano kabla ya uchaguzi ndivyo ilivyopangwa huku akiweka wazi sasa ni wakati wa rufaa na kupelekana kamati ya maadili.

“Siku tano kabla ya uchaguzi ndio tarehe iliyopangwa tangu taratibu kuelekea uchaguzi huo zimeanza taarifa za kuhofia fujo kwa wagombea ndio kwanza nazisikia kutoka kwako sijajua kama linaukweli au la,” alisema.