Viwanja Ligi Kuu gumzo

Muktasari:

  • Viwanja vinavyotumika ni Taifa, Uhuru na Azam Complex ( Dar es Salaam), Mkwakwani, Tanga, Sokoine Mbeya, Kambarage, Mwadui Complex (Shinyanga), Kaitaba Bukoba, CCM Kirumba na Nyamagana Mwanza.

Dar/Mikoani.Licha ya Ligi Kuu Tanzania Bara kushirikisha timu 20, lakini hali mbaya ya viwanja imeonekana kupunguza ubora wa mashindano hayo.

Pia ubovu wa idadi kubwa ya viwanja katika eneo la kuchezea vimeonekana kuwa moja ya chanzo cha wachezaji wengi kupata majeraha ya mara kwa mara.

Mbali na eneo la kuchezea, viwanja hivyo havina mazingira bora katika maeneo mbalimbali yakiwemo vyoo, vyumba vya kuvalia nguo na majukwaa.

Viwanja vinavyotumika ni Taifa, Uhuru na Azam Complex ( Dar es Salaam), Mkwakwani, Tanga, Sokoine Mbeya, Kambarage, Mwadui Complex (Shinyanga), Kaitaba Bukoba, CCM Kirumba na Nyamagana Mwanza.

Mazingira ya uwanja yasiyokuwa rafiki hasa eneo la kuchezea yamechangia kwa namna moja au nyingine kufifisha vipaji vya wachezaji kwa kuhofia kupata majeraha.

Pia baadhi ya timu zinashindwa kupata matokeo mazuri kwa kuwa makocha wanalazimika kubadili programu na kutumia mbinu mbadala kulingana na mazingira yasiyoridhisha ya uwanja.

Licha ya Uwanja wa Nyamagana kuwekwa nyasi za bandia na kuboreshwa kwa vyumba vya kuvalia nguo, lakini vyoo ni tatizo kubwa kwa mashabiki.

Baadhi ya wadau nchini wametoa maoni tofauti kuhusu ubovu wa viwanja vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Msaidizi wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA) Khalid Bitebo ‘Zembwela’ alisema wamejipanga vyema kuboresha usafi kabla na baada ya mchezo.

Alisema mabadiliko ya ratiba yamechangia kutoa tafsiri mbaya kwa wadau wa soka na alitoa mfano kwa mchezaji Adeyum Saleh aliyeanguka katika mchezo dhidi ya Mbao ambapo beki huyo aliwahishwa hospitali kwa kutumia gari binafsi.

“MZFA hatukujua mapema kama mechi imepangwa kuchezwa saa nane mchana ndio maana hatukufanya maandalizi ya kutosha,” alisema Bitebo.

Tofauti na alivyosema Bitebo, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Shinyanga (Shirefa) Bevin Kapufi alidai uchafu uliopo Uwanja wa Kambarage unatokana na uchache wa wafanyakazi.

Wasikie Makocha

Kocha wa Prisons, Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema Tanzania Bara ina viwanja vitatu vyenye hadhi ya kutumika kwa Ligi Kuu ni Taifa, Kaitaba na CCM Kirumba.

“Mpira haupigwi bali unachezwa sasa mtachezaje kwa viwanja kama hivyo maana inabidi msicheze mpira mpige tu ili uondoke eneo lako maana ukizembea unaweza utajikuta unajifunga mwenyewe,”alisema Rishard.

Kocha wa Ndanda Khalid Adam alisema Uwanja wa Nangwanda ni mzuri katika eneo la kuchezea na haoni tatizo kwa wachezaji wazawa kutumia viwanja hivyo.

Kauli ya daktari

Daktari wa Azam Mwanandi Mwankemwa alisema uwanja wa Kaitaba ndio bora kulinganisha na vingine. Pia alisema Taifa na Samora zenye nyasi za kawaida zina sifa ya kuchezewa kwa mechi za Ligi Kuu.

“Viwanja vya nyasi bandia chini wanaweka mawe na simenti kabla ya kupachikwa majani ya plastiki, kadri unavyotumia majani yanazidi kukatika. Wachezaji wengi wanapatwa na matatizo ya kifundo cha mguu na magoti,” alisema Mwankemwa.

Tamko la TFF

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao alisema wako katika mpango wa kukarabati viwanja vinavyotumika kwa Ligi Kuu.