Viungo Simba tishio

Muktasari:

Ikiwa watapangwa kama mawinga wanapaswa pia kujiandaa na ushindani kutoka kwa Miraji Athumani na Deo Kanda ambao kiasili ni mawinga.

Dar es Salaam. Safu ya kiungo ni eneo linaloonekana linaweza kuwa mhimili na chachu ya mafanikio ya Simba katika mashindano ya msimu ujao.

Uwepo wa nyota wanane wanaomudu kucheza safu ya kiungo unalipa uhakika benchi la ufundi kutumia mifumo na mbinu tofauti uwanjani kulingana na ubora wa timu pinzani.

Nyota wanane waliopo Msimbazi ni Said Ndemla, Sharaf Shiboub, Hassan Dilunga, Francis Kahata, Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, Clatous Chama na Mzamiru Yassin.

Katika kundi hilo Mzamiru, Mkude, Shiboub na Ndemla wanamudu kucheza vyema kama viungo wakabaji.

Lakini bado Ndemla, Mzamiru na Shiboub wanaweza kucheza pia nafasi ya kiungo namba nane kutegemeana na mahitaji ya kiufundi ya mechi husika.

Ubora huo unachagizwa na uwepo wa Ajibu, Dilunga, Kahata na Chama wanaoweza kucheza kama viungo washambuliaji kulingana na mfumo ambao timu hiyo itaamua kuutumia.

Endapo benchi la ufundi litatumia mfumo wa 4-4-2, maana yake wataanza viungo wawili tu kati ya wanane, mmoja akicheza namba nane na mwingine sita ingawa kutokana na Ajibu, Dilunga na Chama kuwa na uwezo wa kucheza pia kama mawinga huenda wakajikuta wakipangwa pembeni kama mawinga.

Ikiwa watapangwa kama mawinga wanapaswa pia kujiandaa na ushindani kutoka kwa Miraji Athumani na Deo Kanda ambao kiasili ni mawinga.

Ajibu na Chama wanaweza kupangwa nafasi ya mshambuliaji wa pili katika mfumo huo ingawa hilo linaweza kuwa gumu kutokana na uwepo wa washambuliaji asilia kama Meddie Kagere, John Bocco na Wilker da Silva.

Kama benchi la ufundi litatumia mfumo wa 4-2-3-1, maana yake watano kati ya wanane wanaweza kuanza kwa pamoja ambapo kutakuwa na viungo watatu wa juu ambao watakuwa na jukumu la kumlisha mshambuliaji mmoja atakayesimama mbele au hata wenyewe kushiriki katika kufunga mabao pamoja na viungo wawili watakaocheza mbele ya mstari wa mabeki.

Mfumo unaoweza kuwafanya angalau saba kati yao waanze kwa pamoja ni 4-3-3, ambao wawili kati ya Shiboub, Dilunga au Kahata wanaweza kupangwa kama viungo ushambuliaji mbele ya kiungo mkabaji, wakati Ajibu na Chama wakianza kama washambuliaji wa pembeni.

Lakini pia kutokana na uwezo wa baadhi ya viungo hao kumudu kucheza nafasi tofauti uwanjani, hata mfumo wa 3-4-3 unaweza kuwapa nafasi ya kucheza kundi kubwa la viungo hao.

Usajili wa Ajibu kutoka Yanga unaweza kuongeza kitu zaidi Simba kwa kuipa faida ya kuwa na mpango mbadala wa kupika mashambulizi na mbinu za kusaka bao langoni mwa timu pinzani. Ajibu ndiye aliyetengeneza idadi kubwa ya mabao aliyofunga nyota wa zamani wa Yanga Heritier Makambo.

Uwezo wa nyota huyo kupiga pasi za juu kwenda kwa washambuliaji, unaweza kuwa na faida kwa Simba na hasa washambuliaji John Bocco na Kagere ambao msimu uliopita walifunga idadi kubwa ya mabao kwa kutumia miguu badala ya vichwa licha ya kuwa warefu kiumbo.

Pia kundi hilo kubwa la viungo pamoja na uwezo wa baadhi yao kucheza nafasi nyingi tofauti uwanjani huenda ikawa faida kwa Simba kwa kulipa nafasi benchi lake la ufundi kufanya mzunguko wa kikosi ili kuwalinda nyota wake wasipate uchovu kutokana na ushiriki wake kwenye mashindano manne tofauti ambayo ni Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu, Kombe la FA na Kombe la Mapinduzi.

Kahata ambaye amesajiliwa na Simba akitokea Gor Mahia, alitamba kuwa yupo tayari kupigania nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

“Napenda changamoto popote ninapokuwa, hivyo naweza kusema sina neno kubwa zaidi ya kupenda ushindani wa namba hata huko Simba na kokote sitaweza kuogopa changamoto,” alisema Kahata. Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema kila mchezaji ana umuhimu wake kutegemeana na kocha atakavyomtumia.

“Kwa vile kocha ndiye amewapendekeza tusubiri kuona namna atakavyopanga kikosi kwa mtazamo wangu, viungo hao ni wazuri kila mmoja ana ubora wake,” alisema Pawasa.