Vita ya ufungaji bora TPL

Muktasari:

  • Makala haya yanakuletea tathmini ya wachezaji saba ambao miongoni mwao, mmoja anaweza kuibuka kuwa mfungaji bora kutokana na namna ligi ilivyo.

Ligi Kuu Tanzania Bara inazidi kushika kasi ikikaribia theluthi ya mwisho huku timu zikiendelea kusaka pointi za kuziwezesha kutimiza malengo zilizojiwekea msimu huu.

Zipo timu ambazo zinapambana kusaka ubingwa wa ligi lakini kuna nyingine ambazo zenyewe zinapigania kubaki kwenye ligi.

Hata hivyo, wakati timu zikiwa kwenye vita ya kuwania pointi, kuna ushindani mwingine ambao ni wa kuwania zawadi ya ufungaji bora kwenye Ligi Kuu msimu huu ambayo inahusisha nyota kutoka klabu tofauti zinazoshiriki kwenye ligi.

Wapo ambao wanaonekana wana nafasi kubwa ya kufanikiwa kuondoka na tuzo hiyo ya mfungaji bora, pia wapo ambao hawaonyeshi wanaweza kuhimili vita ya ushindani ya kuwa kinara katika ufungaji.

Makala haya yanakuletea tathmini ya wachezaji saba ambao miongoni mwao, mmoja anaweza kuibuka kuwa mfungaji bora kutokana na namna ligi ilivyo.

Salum Aiyee - Mwadui 6/10

Mshambuliaji wa Mwadui FC ambaye wengi walikuwa hawamfahamu lakini jina lake limeanza kuwa midomoni na akilini mwa mashabiki wa soka baada ya kushika usukani katika mbio za kuwania ufungaji bora akiwa na mabao 15.

Hata hivyo licha ya kuwa anaongoza kufumania nyavu, ana kazi kubwa ya kufanya kupambana na mastraika wa timu nyingine hasa wa Simba na Yanga ambao wanamnyemelea kwa kasi.

Kama akiwa na juhudi, anaweza kuandika historia kwani timu yake imeshamaliza mechi dhidi ya timu kubwa na imebakiza dhidi ya zile za kawaida jambo linaloweza kuwa faida kwake.

Heritier Makambo-Yanga 8/10

Amefanya kazi kubwa katika kuifanya Yanga ikae kileleni mwa msimamo wa ligi kupitia mabao yake 12 aliyoifungia timu hiyo hadi sasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Makambo ana uwezekano mkubwa wa kubeba kiatu cha ufungaji bora kutokana na aina ya mabao ambayo amekuwa akifunga.

Ni hatari kwa mabao ya vichwa na kutokana na udhaifu wa mabeki wengi wanaoshiriki Ligi Kuu katika kuokoa mipira ya krosi na kona, basi anaweza kufunga mabao ya kutosha kwenye mechi 11 za Yanga zilizobakia.

Hata hivyo, changamoto kubwa inayomsumbua Makambo ni kutokuwa na mwendelezo mzuri wa ufungaji, pia amekuwa hafungi idadi kubwa ya mabao kwa kutumia miguu.

Meddie Kagere-Simba 9/10

Kama asipopatwa na majeraha au kuporomoka kiwango, Kagere mwenye mabao 12 ni wazi ndiye mchezaji anayepewa nafasi ya kutwaa kiatu hicho.

Amekuwa hana mzaha anapokuwa mbele ya lango. Anafunga kwa staili tofauti ikiwemo kwa kutumia kichwa na miguu yote miwili, anabebwa na uwepo wa idadi kubwa ya wachezaji wanaojua kuchezesha timu ndani ya kikosi cha timu yake.

Kubwa zaidi, kitendo cha Simba kuwa na idadi kubwa ya mechi mkononi, kinamweka katika nafasi kubwa ya kuwa mfungaji bora.

Simba imebakiza mechi 18 dhidi ya timu za Prisons, Biashara United, Kagera Sugar, Coastal Union, Alliance, Mbao, Azam, Mbeya City, KMC, Mtibwa, Ndanda, JKT Tanzania, Ruvu Shooting na Singida United.

Dickson Ambundo-Alliance 5/10

Timu yake imebakiza mechi tisa dhidi ya timu za Ruvu Shooting, Stand United, Biashara United, Mwadui, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Singida United, Coastal Union na Simba

Ambundo hata hivyo ana mlima mrefu wa kupanda ili awe mfungaji bora kwani kucheza nafasi ya winga wa pembeni kunamfanya awe mbali ya lango tofauti na wenzake ambao wengi wanacheza nafasi ya mshambuliaji wa kati.

John Bocco-Simba 8/10

Hakuanza vizuri msimu huu lakini katika siku za hivi karibuni amekuwa moto wa kuotea mbali na taratibu ameonekana kuanza kurudisha makali ya kufumania nyavu huku akitengeneza safu kali ya ushambuliaji na Kagere.

Hata hivyo, uwepo wa Kagere unaweza kumfanya Bocco asiibuke mfungaji bora kwani mara kwa mara nahodha huyo wa Simba ndio huwa mpishi wa mabao ya mshambuliaji mwenzake.

Pamoja na hayo, Bocco ananufaika na uteuzi wa yeye kuwa mpigaji penati chaguo la kwanza ndani ya kikosi cha Simba jambo ambalo ni faida kwake katika mbio hizo.

Ayoub Lyanga-Coastal Union 6/10

Ni mshambuliaji hatari ambaye ana uwezo mkubwa wa kufumania nyavu, kutengeneza nafasi na kupambana na mabeki wa timu pinzani.

Ana nguvu, akili na uwezo wa kumiliki mpira na kupiga chenga sifa ambazo zimemwezesha kufunga mabao tisa hadi sasa.

Timu yake imebakiza mechi tisa ambazo ni dhidi ya Singida United, Prisons, Mtibwa Sugar, Mbeya City, Simba, Ndanda FC, Stand United na Alliance

Donald Ngoma-Azam 7/10

Alikosa idadi kubwa ya mechi za mwanzo kutokana na majeraha ambayo yalimfanya akose baadhi ya mechi za mwanzo za Azam FC.

Hata hivyo baada ya kupona na kuwa fiti, Ngoma amekuwa akiibeba timu hiyo kutokana na mabao ambayo amekuwa akiyafunga pamoja na pasi za mabao anazowapigia wenzake.

Licha ya kuwa amefunga mabao saba, anaonekana ni mchezaji tishio kwenye vita ya ubingwa hasa ukizingatia kuwa timu yake ina mechi 11 mkononi dhidi ya timu za Simba, Yanga, Mtibwa, KMC, Stand United, Mbao FC, Kagera Sugar, Singida United, Mbeya City na Ndanda.