Vita ya ufungaji bora Aiyee, Makambo wafunguka

Muktasari:

 

  • Hadi sasa Salim Aiyee (Mwadui FC) ndiye anaongoza kwa mabao 13, huku Heritier Makambo (Yanga) akifuatia akiwa na 12 na Meddie Kagere (Simba) na Said Dilunga wa Ruvu Shooting wakiwa na 10 kila mmoja.

Mwanza. Achana na ushindi mabao 2-1, walioupata Yanga jana dhidi ya Mbao FC ishu ilikuwa kwa nyota wake Heritier Makambo aliyefunga bao lake la 12 na kukoleza ushindani wa kuwania mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu.

Katika mbio hizo za ufungaji mshambuliaji wa Mwadui, Salim Aiyee anaongoza akiwa na mabao 13, akifuatiwa na  Makambo (12) na Meddie Kagere (Simba) na Said Dilunga wa Ruvu Shooting wakiwa na mabao 10 kila mmoja.

Mshambuliaji Aiyee ameweka bayana lengo lake msimu huu ni kuwa mfungaji bora ili kuweka historia mpya katika kazi yake ya soka.

 Alisema kujituma kwake, nidhamu ya mchezo pamoja na ushirikiano walionao ndani ya timu ni moja ya mambo yanayompa hamasa na mwanga katika kufikia malengo yake msimu huu na kwamba atakuwa makini anapokuwa uwanjani kuzitumia vyema nafasi anazopata.

 “Makambo na wenzake lazima wajipange tu, msimu huu napambana kadri ya uwezo wangu kuhakikisha nabeba tuzo ya kiatu cha mfungaji bora, naamini kwa ushirikiano wetu, nidhamu ya mchezo na kumtanguliza Mungu itanisaidia kufikia malengo yangu,” alisema Aiyee.

Kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu alisema kutokana na kujituma kwa nyota wake huyo huenda neema ikamshukia hapo mbeleni.

“Kwa ujumla anapambana na akiendelea hivi anaweza kuwa mfungaji bora kwa msimu huu, ana bidii na nidhamu kwahiyo kikubwa ni kuendelea kufuata maelekezo na kufanya kile anachostahili bila kuwaogopa wale wa Simba na Yanga,” alisema Bizimungu.

Hata hivyo, Makambo ni kama alimjibu Aiyee kwani ndani ya dakika 50 za mchezo wao na Mbao jana alifunga bao Yanga ikishinda 2-1.

Makambo alisema ufupi lolote linawezekana katika mbio za ufungaji bora kutokana na kwamba Ligi bado inaendelea ni mapema kulizungumzia hilo isipokuwa kikubwa ni kupambana.

“Lolote linawezekana kwa sababu ligi bado haijaisha kwahiyo ni mapema kuzungumzia hilo, kikubwa ni kupambana katika mechi zilizobaki kuhakikisha nafunga mabao japo ligi ni ngumu,” alisema Makambo.