Vita ya makipa wa Afcon 2019

Muktasari:

Tulia mwanangu nikupatie udaku kutoka kwenye Social Media. Baada ya zile shinikizo za kumtaka Kocha wa Stars, Mfaransa Sebastien Migne, amfikirie Dennis Oliech, moto umehamia kwa ‘Kenya One’.

TIMU ya Taifa Harambee Stars, imeshaanza maandalizi kabambe kwa ajili ya makala ya 32 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2019), yatakayotimua vumbi kuanzia Juni 15 hadi Julai 13, nchini Misri, baada ya waandaaji wa awali Cameroon, kupokonywa haki ya kuandaa kutokana na maandalizi yasiyoridhisha.

Maandalizi hayo kama kawaida yameambatana na tambo na mchecheto kutoka kwa mashabiki wa soka, ambao kila mara hutumia mitandao ya kijamii kutoa dukuduku lao. Katika pitapita zangu kwenye baadhi za kurasa za Spoti za Facebook na Twitter, nimekutana na mjadala kuhusu ‘Kenya One’.

Unajua nazungumzia nini? Tulia mwanangu nikupatie udaku kutoka kwenye Social Media. Baada ya zile shinikizo za kumtaka Kocha wa Stars, Mfaransa Sebastien Migne, amfikirie Dennis Oliech, moto umehamia kwa ‘Kenya One’.

Ni hivi, baada ya Bonface Oluoch kuisaidia Gor Mahia kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, mashabiki hao, wengi wao wakiwa ni wale kutoka Jeshi la Kijani (Gor Mahia), wameanza kuwachambua makipa wetu mazee. Katika makala haya tunakuletea majina ya makipa wanne, wanaogonganisha vichwa. Nani atasimama langoni huko Misri?

Patrick Matasi (St. Georges, Ethiopia)

Patrick Matasi (31), ndio kipa bora nchini Kenya kwa sasa, hilo halina ubishi. Kipa huyu aliyejiunga na klabu ya St. Georges ya Ethiopia, kwa mkataba wa miaka miatatu, ndiye macho ya Kocha Migne kwa sasa. matumaini ya Wakenya yako kwake.

Matasi ambaye ni mchezaji wa zamani wa Kabrass United, AFC Leopards, Posta Rangers na Tusker, mpaka sasa ameshaichezea Harambee Stars mechi 17 tangu mwaka 2017 na ndiye aliyesimama langoni katika mechi zote za Kundi F na kushuhudia Kenya ikifuzu AFCON kwa mara ya kwanza baada ya miaka 14.

Lakini licha ya kuonekana kutokuwa na mpinzani, ukweli, Matasi ana kazi kubwa ya kupambana na upinzani kutoka kwa Shikhalo na Oluoch, anayeonekana kupigiwa upatu mkubwa kuchukua nafasi katika lango la Harambee Stars, katika makala haya ya 32 yatakayofanyika nchini Misri.

Bonface Oluoch (Gor Mahia)

Kwa muda mrefu sana, tangu ‘Kenya One’ Francis Onyiso atundike daluga, Kipa wa Gor Mahia, ambaye alipitia katika mikono ya Onyiso, amekuwa akisimama katika lango la Harambee Stars, kwenye michuano mbalimbali tangu mwaka 2010, akicheza mara 26.

Oluoch ambaye anakipiga katika klabu ya Gor Mahia, ambao ni mabingwa watetezi wa KPL na wawakilishi wa Kenya katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, bila ubishi ni mmoja wa vipaji vya soka vinavyotawala anga la soka la Kenya.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, Kipa huyu mwenye umri wa miaka 32, alijikuta akipoteza nafasi yake katika kikosi cha Kogalo, akishindwa kupambana na damu changa, Fredrick Odhiambo na Shaban Odhoji.

Oluoch pia amekutana na upinzani mkubwa kutoka kwa damu changa kwenye kikosi cha Harambee Stars. Akaishia kusugua benchi, nafasi yake ikigombaniwa na Patrick Matasi, Brian Bwire na Farouk Shikhalo.

Lakini kwa kuwa hakuna kijiji kisichokosa wazee, kuna kila dalili za Oluoch, kutokana uzoefu wake, akawaweka benchi makipa wengine na kusimama langoni, kwenye fainali za mwaka huu za Kombe la Mataifa ya Afrika. Kwa nini hilo lishindikane wakati tayari ameshaonyesha uwezo na nia ya kuimarika?

Januari 20, Kogalo ikiwa na faida ya ushindi wa 2-1, iliyoipata katika mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho, Kocha wa Gor Mahia, Hassan Oktay, aliamua kufanya maamuzi magumu ya kumpanga Bonface Oluoch katika kikosi chake, badala ya Fredrick Odhiambo.

Oktay hajutii kumwamini Oluoch. Akiwa langoni huko Doula Cameroon, Ouoch alihakikisha Kogalo inatiga hatua ya makundi na kuitupa nje New Stars De Doula, huku akichomoa michomo kadhaa na kuongoza Kogalo kulazimisha sare ya 0-0 ugenini.

Farouk Shikhalo (Bandari FC)

Kwa sasa hakuna kipa wa kufananisha naye, hasa kwa wachezaji wa ndani. Ukimwacha Patrick Matasi, hakuna anayemkaribia Shikhalo kwa ubora na huo ndio ukweli. Katika kikosi cha Stars, Mlinda lango huyu wa Bandari mwenye miaka 24, ni namba mbili nyuma ya Matasi. Msimu uliopita alitawazwa kuwa Kipa bora wa KPL, baada ya kuandikisha ‘cleen sheets’ 17 huku akiisaidia Bandari kumaliza katika nafasi ya pili kwenye jedwali nyuma ya mabingwa Gor Mahia.

Unavyosoma makala haya, yupo na timu yake Jijini Dar es salaam, chini ya ukufunzi wa Bernard Mwalala, kusaka ubingwa wa Kombe la SportPesa, linaloendelea nchini Tanzania, ikiwa ni mara yao ya kwanza kushiriki.

Kipa huyo wa zamani wa Tusker FC, Muhoroni Youth na Posta Rangers, huenda akamwondoa Matasi langoni huko Misri. Hapa ndipo vita yenyewe ilipo, Matasi yuko fiti na Shikhalo naye yupo fiti, uamuzi anatafanya Migne.

John Oyemba (Kariobangi Sharks)

John Oyemba ambaye anaonekana kuimarika kila uchao, hasa baada ya kumpokonya nafasi Brian Bwire, kwenye lango la Kariobangi Sharks, naye ni Kipa mwengine ambaye kwa sasa anampa Kocha wa Stars, Sebastien Migne mtihani wa kufanya maamuzi.

Kipa huyo yupo katika kikosi cha Sharks, Jijini Dar es Salaam, kusaka ubingwa wa Kombe la SportPesa, huu ukiwa ni msimu wao wa tatu na vijana hao wa William Muluya wanapigiwa upatu kuibuka mabingwa.