Vita ya buti la dhahabu

Muktasari:

Vita ya kusaka Kiatu cha Dhahabu imezidi kunoga na pengine kutakuwa na mchuano mkali tofauti na msimu uliopita. Kwenye msimu uliopita, mastaa watatu walipewa tuzo hiyo, ambapo staa wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang na wawili wa Liverpool, Sadio Mane na Mohamed Salah, ambapo kila mmoja alifunga mabao 22.

LONDON, ENGLAND . JURGEN Klopp ameshafunga mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Ubora wa kikosi chake cha Liverpool umewapoteza kabisa wapinzani wake Pep Guardiola, Jose Mourinho, Ole Gunnar Solskjaer, Mikel Arteta, Frank Lampard na Brendan Rodgers, hivyo wasubiri tu mwakani.

Chama la Klopp, Liverpool limeweka pengo la pointi 16 kileleni kwenye msimamo wa ligi dhidi ya Manchester City ya Guardiola inayoshika nafasi ya pili. Ameiacha Leicester City ya Rodgers kwa pointi 19 kwenye nafasi ya tatu na pointi 27 dhidi ya Chelsea ya Lampard kwenye nafasi ya nne huku Solskjaer na chama lake la Man United ameachwa kwa pointi 34. Mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, Klopp ameshazimaliza.

Na pengine sasa zimebaki mbili tatu kuwania kuwamo kwenye Top Four, kupambana kutoshuka daraja na mbio ya tatu ni ile ya kusaka Kiatu cha Dhahabu kwenye ligi hiyo. Hapo kwenye Top Four, mambo yanaweza kubaki kama yalivyo kama Man United, Spurs na Arsenal hazitabadilika. Shughuli ipo kwenye kushuka daraja, lakini mambo mazito zaidi yapo kwenye kuwania Kiatu cha Dhahabu.

Vita ya kusaka Kiatu cha Dhahabu imezidi kunoga na pengine kutakuwa na mchuano mkali tofauti na msimu uliopita. Kwenye msimu uliopita, mastaa watatu walipewa tuzo hiyo, ambapo staa wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang na wawili wa Liverpool, Sadio Mane na Mohamed Salah, ambapo kila mmoja alifunga mabao 22.

Staa wa zamani wa Chelsea, Eden Hazard alinyakua tuzo ya kupiga asisti nyingi ambapo alipiga 15, huku kipa wa Liverpool, Alisson Becker alishinda Golden Glove baada ya kucheza mechi 21 za ligi bila ya kuruhusu mpira kwenye ligi.

Baada ya kuona Liverpool imeshajisogeza kwenye taji, sasa mastaa waliopo kwenye ligi hicho mchuano wao mkali upo kwenye kushindana kufunga ili kunyakua Kiatu cha Dhahabu. Msimu bado kuna mechi 14 mbele za kucheza, hivyo kutoka sasa hadi mwisho kuna kitu chochote kinachoweza kutokea.

Kwa sasa straika wa Leicester City, Jamie Vardy, ndiye anayeongoza, akiwa ametikisa nyavu mara 17, lakini nyuma yake yupo staa wa Man City, Sergio Aguero, ambaye amefunga mabao 16. Aubameyang yupo kwenye nafasi ya tatu, akiwa amefunga mabao 14, akikabana koo na wakali wengine, Danny Ings wa Southampton na Marcus Rashford wa Man United.

Kinda wa Chelsea, Tammy Abraham hayupo mbali sana akiwa amefunga mabao 13, huku wakali wengine walioshinda tuzo hiyo misimu ya karibuni, Mo Salah, Mane na Harry Kane wa Spurs, ambaye kila mmoja amefunga mabao 11. Hiyo ni kwenye vita ya kusaka Kiatu cha Dhahabu.

Kwenye wanaochuana tuzo ya asisti mambo ni moto, huku Kevin De Bruyne wa Man City akiongoza kwa kupiga 17, tano zaidi ya mtu anayemfuatia ambaye ni beki wa pembeni wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold. Kisha wanafuatia mastaa wawili wa Man City, Riyhad Mahrez na David Silva, ambapo kila mmoja amepiga asisti tisa sawa na staa wa Spurs, Son Heung-Min huku Mane akihusika kwenye asisti nane.

Mchuano mkali zaidi upo kwenye tuzo ya Golden Glove, ambapo kuna makipa watano wamecheza idadi sawa ya mechi ambazo hawakuruhusu nyavu zao kuguswa, ambapo ni Kasper Schmeichel wa Leicester City, Dean Henderson wa Sheffield United, Ben Foster wa Watford, Nick Pope wa Burnley na anayetetea tuzo hiyo, Alisson, ambapo wote hao wameshuhudia mechi nane wakicheza bila ya nyavu zao kuguswa, huku Ederson wa Man City akicheza mechi saba.