Vita mshindi wa pili VPL bado ngumu, Simba yapewa heshima Mtwara

Sunday July 5 2020

 

By THOBIAS SEBASTIAN NA ELIYA SOLOMONI

TIMU kongwe za hapa nchini Simba na Yanga ni kama zimetegeana katika mechi zao za Ligi Kuu Bara ambazo wamecheza leo Jumapili Julai 5 katika viwanja tofauti.

Yanga waliokuwa ugenini kucheza dhidi ya Biashara United, mechi yao imemalizika kwa suluhu na kuweka rekodi ya kuvuna pointi moja kwa mara ya kwanza katika uwanja wa CCM Karume mkoa wa Mara kwani walishindwa kufanya hivyo msimu uliopita.

Yanga walionekana kuanza katika kiwango cha chini kuliko wapinzani wao Biashara United pengine ni baada ya kuumia kwa kiungo fundi, Haruna Niyonzima ambaye alitoka dakika ya 8, kipindi cha kwanza na nafasi yake kuingia Abdulaziz Makame 'Bui'.

Baada ya Niyonzima kutoka Yanga walionekana kukosa ubunifu na haswa pindi walipokuwa wanashambulia kuwa na mpira kwani walikuwa wakipoteza kwa kunaswa na wachezaji wa Biashara United na hata kushindwa kufanya mashambulio ya maana dakika zote 45, za kipindi cha kwanza.

Wakati Yanga wakionekana kushindwa kucheza vizuri katika kipindi cha kwanza wapinzani wao Biashara kama wangekuwa makini wangefunga bao la kuongoza kwani walitengeneza nafasi tatu za wazi lakini walishindwa kuzitumia baada ya mbili kutoka nje na moja kupanguliwa na kipa Farouk Shikhalo.

Katika kipindi cha pili Yanga baada ya kufanya mabadiliko ya kuwatoa Kelvin Yondani, Ditram Nchimbi, Feisal Salum na Deus Kaseke huku nafasi zao zikichuliwa naMrisho Ngassa, Patrick Sibomana, Tariq Seif na Erick Kabamba walionekana kuimalika na kucheza vizuri kuliko kipindi cha kwanza.

Advertisement

Yanga walionekana kuimarika kwa kufanya mashambulizi ya hatari ikiwemo faulo iliyopigwa na Sibomana dakika 76, ambayo ilikwenda kugonga goli la Biashara United na kumkosa mchezaji mwengine wa kumalizia kabla ya shambulizi hilo kuokolewa.

Yanga waliendelea kuimalika mbali ya kufanya mashambulizi ya mara kwa mara ambayo yaliokolewa na wachezaji wa Biashara ambao walionekana kuwa fiti kwa kutumia zaidi nguvu waliweza kutawala mpira tofauti na kipindi cha kwanza walipokuwa wanapoteza mara kwa mara.

Kwa upande wa Biashara wao walionekana kuwa na nidhamu kubwa pindi walipokuwa na mpira walikwenda kushambulia kwa pamoja kama timu huku safu yao ya ushambuliaji ilikuwa ikiongozwa na Ramadhani Chombo 'Ridondo' na Atupele Green ambao walionekana kuwa mwiba kwa mabeki wa Yanga kwani walikuwa wakiwasumbua mara kwa mara.

Wachezaji wa Biashara waliendeleza nidhamu hiyo hata kwenye kuzuia mashambulizi ya Yanga kwani walikuwa wanatumia nguvu na hata wakati mwingine kucheza rafu nyingi kwenye maeneo tofauti ya uwanja, jambo ambalo liliwafanya baadhi ya wachezaji wa wapinzani wao kuingiwa na uoga.

Kwa matokeo hayo Yanga wamefikisha pointi 61, wakicheza mechi 33.

Biashara United wao matokeo hayo yaliwafanya kufikisha pointi 45, na kupanda nafasi ya tisa wakimshusha Tanzania Prison waliokuwa katika nafasi hiyo na pointi 44.

 

Wakati huo huo katika uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara kulikuwa na mechi nyingine kati ya Ndanda waliowakaribisha mabingwa wa ligi Simba.

Baada ya piga nikupige za kipindi cha kwanza, timu hizo zilirejea kipindi cha pili kukiwa hakuna mabadiliko yoyote.

Dakika ya 56, Ndanda walipoteza nafasi ya kuitangulia Simba baada ya kuchongwa krosi kutoka upande wa kulia, Omary Mponda alijitwisha kichwa ambacho kilitemwa na Aishi Manula wakati ambao mabeki wakizubaa mpira ule ukamkuta Abdul ambaye alipiga shuti na Manula alilicheza tena.

Ndanda walionekana kurejea na nguvu ile ile waliyoanza nayo kipindi cha kwanza huku wakiwategemea Kigi Makasi,Taro Fonald na Abdulrazack Mohammed kuchezesha timu katika eneo lao la kati la uwanja.

Dakika ya 66, yalifanyika mabadiliko ya kwanza katika mchezo huo ambapo yaliwahusu Simba kwa kumtoa Wawa na nafasi yake akaingia kiraka, Erasto Nyoni ambaye hata katika mchezo uliopita wa kombe la FA dhidi ya timu yake ya zamani, Azam FC alianzia benchi.

Simba walifanya tena mabadiliko dakika mbili baadaye kwa kutoka John Bocco na kuingia kinara wa mabao Ligi Kuu Bara, Meddie Kagere ambaye hivi karibuni kasi yake ya ufungaji imeonekana kupungua.

Dakika ya 71, Simba walifanya tena mabadiliko ya kutoka Luis Miquissonena kuingia Said Ndemla, dakika moja baadaye akatoka kiungo wa Kibrazil, Fraga na akaingia Mzamiru Yassin.

Ndanda nao walifanya mabadiliko ya kumtoa Omary Mponda na kuingia Omary Ramadhan aliyevalia jezi namba saba mgongoni ili akaongeze nguvu katika safu yao ya ushambuliaji.

Dakika ya 80, wakafanya tena mabadiliko ya kumtoa Vitalisy Mayanga na kuingia Hussein Javu huku Simba wakimaliza hesabu katika mabadiliko kwa kumtoa Chama na kuingia Hassan Dilunga.

Pamoja na timu zote mbili kufanya mabadiliko hayo hadi dakika 90 za mchezo huo hapakuwa na timu iliyopata bao hivyo walilazikima kugawana pointi moja moja.

Kabla ya kuanza mchezo huo Ndanda ambao ni wenyeji, iliwalazimu kujipanga katika eneo la wachezaji kuingilia kukisubiri kikosi cha Simba wakiwa wamejipanga mistari miwili ili kipite kati ikiwa ni ishara wa kuwapa heshima yao.

Ni kawaida kilichotokea kabla ya mchezo kuanza katika Ligi mbalimbali za soka, timu iliyotwaa ubingwa ikiwa na michezo mkonini kupigiwa makofi ya pongezi kwa kile ambacho wamekifanya.

Advertisement