Vita kuepuka kushuka Ligi Kuu kuendelea leo, kesho

Tuesday July 14 2020

 

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Ligi Kuu inaendelea kwa michezo mitatu leo, huku sita ikichezwa kesho kusaka alama tatu hasa kwa timu zinazokwepa kushuka daraja.

Lipuli inayoshika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi itakuwa nyumbani katika Uwanja wa Samora mjini Iringa kuikaribisha KMC ambazo zinazisaka alama tatu ili kupanda juu.

Mwadui FC yenye alama 40 haina amani kwenye nafasi ya 14 itacheza na Ruvu Shooting wakati Biashara United ikiikaribisha Polisi Tanzania inayosaka nafasi tano za juu.

Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Frank Likwaro alisema wachezaji wametoa ahadi ya kupata ushindi ili wapande juu kwenye msimamo wa ligi.

“Wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo dhidi ya Biashara, hivyo kila mmoja atajituma kuhakikisha kuwa timu inapata ushindi ili iweze kujiweka katika mazingira salama na kufikia malengo ya kumaliza nafasi ya tano,” alisema.

Pato Ngonyani ambaye ni mchezaji wa timu hiyo alisema, “hatutawaangusha mashabiki katika michezo inayofuata na tunaanza na Biashara, mchezo utakuwa mgumu lakini tumeshikamana na kusahau matokeo ya nyuma.”

Advertisement

Kesho, Singida United iliyoaga ligi hiyo itacheza na Yanga ambayo juzi ilipokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Simba katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), na Ndanda FC ambayo haina uhakika wa kusalia msimu ujao itacheza na Tanzania Prisons.

Mtibwa Sugar inayojivuta katika nafasi ya 16 ina kibarua mbele ya Azam FC inayotaka kuendelea kubaki nafasi ya pili. Kagera Sugar itacheza na Coastal Union wakati JKT Tanzania ikicheza na Alliance FC, ilhali Namungo FC ikiikaribisha Mbeya City iliyopo nafasi ya 15.

Namungo inasaka pointi tatu ili kusalia nafasi ya nne, huku Mbeya City ikikwepa kushuka daraja katika mchezo utakaokuwa na ushindani mkubwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa. Kocha wa Namungo FC, Hitimana Thierry alisema lengo ni kumaliza ligi wakiwa kwenye nafasi nne za juu.

“Mbeya City ni timu bora, lakini tumejiandaa baada ya kumaliza mchezo uliopita dhidi ya Sahare sasa tumegeukia kwenye ligi, kikubwa tuombe uzima ndio jambo la msingi,” alisema.

Advertisement