Vipigo vya mfululizo Stand vyamkasirisha Mrundi wao

Muktasari:


Stand United imecheza mechi mbili mfululizo ambazo zote wapoteza ambapo walifungwa na Mwadui bao 1-0 kisha Coastal Union mabao 2-0 jambo ambalo kocha wake Amars Niyongabo amesema hatahamishia hasira kwa Ruvu shooting.


VICHAPO walivyopokea Stand United viwili mfululizo ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani vimemchafua Kocha, Armas Niyongabo na kutangaza vita kwa Ruvu Shooting katika mchezo utakaopigwa kesho Jumatano mkoani Pwani.

Timu hiyo ilianza vyema ligi na kuonyesha ushindani mkali hata kwa timu kongwe za Simba na Yanga, imejikuta ilichezea vichapo mfululizo dhidi ya Mwadui kwa bao 1-0, kisha kuloa kwa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Niyongabo alisema uzembe wa mabeki na washambuliaji wake kutotulia ndio iliwapa wakati mgumu kupoteza pointi zote sita katika dimba lao na kwamba mechi ijayo lazima wasahihishe makosa yao.

Aliongeza kuwa alichobaini katika kikosi chake licha ya kucheza vizuri lakini nyota wake walikosa saikolojia ya kulinda ushindi nyumbani na kujikuta wakiambulia maumivu.

“Matokeo ya mechi mbili zilizopita yamenikera, haswa ya Coasta Union tulikosa umakini kwa sababu tulitangulia kufunga lakini wakasawazisha na kutufunga, kwahiyo tunaenda kwa Ruvu Shooting kusahihisha makosa,”alisema Niyongabo.

Kocha huyo Mrundi aliongeza kuwa wanaenda kuwavaa wapinzani wao kwa tahadhari kutokana na kutoka kupoteza mechi mbili kama wao, hivyo watakuwa makini ili kutopoteza mechi hiyo muhimu kwa kila timu.