HUMWAMBII KITU : Vioja vya Sarri na uvutaji wake wa Sigara uwanjani

Muktasari:

  • Hakuwa kocha wa kwanza kuruhusiwa kuvuta. Makocha wenzake wa zamani wa Italia, Gianluca Vialli ambaye ni staa wa zamani wa Chelsea naye aliwahi kuonekana akivuta, sambamba na Kocha wa zamani wa Watford, Walter Mazzarri naye aliwahi kuonekana akivuta.

LONDON, ENGLAND . HAIJAWAHI kutokea Ligi Kuu ya England ikampata kocha mpenda sigara kuliko Kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri. Kwa sasa anateseka pale katika benchi la Chelsea kutokana na eneo hilo kutoruhusiwa kwa uvutaji wa sigara.

Analazimika kutembea na sigara feki ambayo inampa stimu. Fuatilia historia ya Sarri na sigara zake.

Aruhusiwa kuvuta Italia

Mara kadhaa Sarri alionekana akivuta sigara akiwa kando ya benchi la timu yake ya zamani Empoli kisha baadaye Napoli.

Hakuwa kocha wa kwanza kuruhusiwa kuvuta. Makocha wenzake wa zamani wa Italia, Gianluca Vialli ambaye ni staa wa zamani wa Chelsea naye aliwahi kuonekana akivuta, sambamba na Kocha wa zamani wa Watford, Walter Mazzarri naye aliwahi kuonekana akivuta. Zamani sana pia makocha maarufu katika Ligi Kuu ya England, Sam Allardyce na Arsene Wenger nao waliwahi kuonekana wakivuta.

Hatimaye afungiwa kuvuta

Baada ya miaka mingi ya kuruhusiwa kuvuta uwanjani, hatimaye Sarri na makocha wengine waliokuwa na tabia kama hiyo walifungiwa rasmi kutovuta hadharani.

Hapo hapo kwa haraka Napoli ilimtengenezea kibanda ndani ya uwanja karibu na benchi ili aendelee kuvuta akiwa amejificha kidogo. Pamoja na kuruhusiwa kuvuta katika kibanda chake lakini Sarri aliruhusiwa kuvuta akiwa jukwaani kama akitolewa nje. Mwaka 2016 alipelekwa jukwaani baada ya kutolewa na mwamuzi katika pambano dhidi ya AC Milan. Alionekana akiwa huru kupiga sigara zake na watu aliowakuta.

Asafiri na treni ili avute sigara

Imeripotiwa katika pambano moja la Ligi Kuu ya Italia dhidi ya Bologna ugenini, Sarri aliamua kusafiri mwenyewe kwa umbali wa kilomita 500 akitumia treni ili awe huru kuvuta sigara zake.

Wachezaji pamoja na maofisa wengine walisafiri kwa Ndege lakini Sarri aliamua kutumia treni kwa sababu kuna eneo maalumu la wavutaji. Uvutaji wa sigara katika ndege hauruhusiwi katika kipindi chote bila ya kujali aina ya ndege.

Leipzig yamuandaliwa chumba maalumu avute

Kuna wenyeji wengine ni watu wakarimu. Katika pambano la michuano ya Europa dhidi ya Leipzig ugenini, klabu hiyo ya Ujerumani ililazimika kumuandalia Sarri eneo maalumu la kuvuta sigara zake baada ya kupokea maombi kutoka kwa Napoli.

Leipzig ilitengeneza eneo maalumu kwa Sarri kuvuta ndani ya chumba cha kubadilishi nguo cha Napoli. Kwa kiasi fulani ukarimu wao uliwaponza kwa sababu Napoli ilishinda mechi hiyo mabao 2-0 licha ya kufungwa 3-1 katika pambano la kwanza ikiwa nyumbani. Hata hivyo, matokeo hayo yalimaanisha Napoli na Sarri walikuwa wametolewa katika michuano hiyo.

Nahodha wa Napoli, Marek Hamsiki alisikika akisema: “Sarri anapenda sana kuvuta sigara. Sijawahi kuona. Sijawahi kumuona mtu anayevuta sana sigara kama yeye. Asante Mungu kuna baadhi ya mechi hawezi kuvuta.”

Avuta paketi tano kwa siku

Sarri ni mmoja kati ya makocha walioacha majina makubwa akiwa na Napoli. Baada ya kumpoteza Gonzalo Higuian aliyekwenda Juventus alifanikiwa kumgeuza winga mahiri wa Kibelgiji, Dries Mertens kuwa mshambuliaji wa kati.

Hata hivyo, Mertens licha ya kunufaika na uwezo wa kocha huyo lakini amedai hawezi kuwa kocha kwa sababu ni kazi yenye msongo wa mawazo.

“Nikimaliza kucheza soka kamwe sitakuwa kocha. Ni kazi yenye michosho mingi. Sarri ana mawazo mengi? Naweza kusema ndiyo, anavuta pakiti tano za sigara kwa siku. Unaweza kusemaje kuhusu hilo? Alihoji Mertens.

Machi mwaka jana, Rapa maarufu wa Italia, Nasta alitunga wimbo kwa heshima ya Sarri wimbo ulioitwa ‘Come Maurizio Sarri’.

Wimbo huo ulisababisha akutane na Sarri. Kuashiria Sarri ni maarufu kwa tabia hiyo, Nasta alimuomba kocha huyo atie saini katika pakiti lake la sigara kama ambavyo wachezaji au makocha maarufu huwa wanatia saini katika jezi na mipira ya mashabiki.

“Ni kama vile kusainiwa mpira na Maradona. Ni kumbukumbu. Nitalibeba pakiti hili kwa maisha yangu yote,” alisema Rapa huyo.

Sigara bado hazivutiki vema Chelsea

Wakati Chelsea ilipokuwa inahusishwa na Sarri ilidaiwa ilikuwa na mpango maalumu wa kumjengea eneo maalumu ndani ya chumba cha kubadilishia nguo ili aendelee kuvuta sigara zake.

Hata hivyo, mpaka sasa hawajafanya hivyo. Inadaiwa tajiri wa Chelsea, Roman Abramovich alimtaka Sarri aanze kukubali tabia za Kiingereza ikiwemo kuacha kuvuta sigara na kuvaa suti katika mechi.

Mpaka sasa hajaweza kuvaa suti. Katika pambano la kwanza tu la Chelsea dhidi ya Huddersfield nyumbani, Sarri alionekana akitafuna kitu kama sigara huku kama kawaida akiwa hana mpango na suti.

“Kama nikila kile kivutio chenyewe (filter) hapo naweza kupata tatizo,” alitania Sarri Novemba 2017 wakati alipovutwa na kamera akionekana anatafuna kitu kama sigara katika pambano kati ya Napoli dhidi ya AC Milan.

Akumbatia pakiti la Sigara

Baada ya kuonekana akitafuna sigara katika mechi yake ya kwanza, Sarri alizua mtafaruku baada ya kuonekana akiwa ameshikilia pakiti la sigara dhidi ya Arsenal ingawa alikuwa haruhusiwi kuvuta. Katika pambano hilo Chelsea ilishinda 3-2 ingawa Arsenal ilisumbua sana na kukosa mabao mengi.

Sarri alikiri wakati Arsenal ikiwa katika ubora wake ilikuwa ni nafasi nzuri kwake kuvuta sigara kwa ajili ya kujipoza lakini hilo halikuwezekana.

“Dakika 15 za mwisho za kipindi cha kwanza mambo yalikuwa mabaya sana. Nilifurahia mechi kwa dakika 75, sio zile dakika 15. Zile dakika 15 afadhali ningevuta sigara tu,” alisema Sarri.

Jambo hilo lilisababisha waandishi wamuhoji sana kuhusu tabia yake ya kuvuta sigara kwa kasi, na mwenyewe alidai ameacha rasmi kuvuta wakati mechi ikiendelea. “Nitavuta jioni baada ya mechi. Wakati wa mechi sitavuta. Nitasimama kwa mwaka mmoja au miwili baada ya hapo nitaanza tena.”