Vinara Ligi Kuu mtegoni

Muktasari:

Kagera itacheza na Yanga SC kesho, wakati Simba SC ikiikaribisha Biashara United keshokutwa.

Dar es Salaam. Timu nne zinazoongoza msimamo wa Ligi Kuu, zinakabiliwa na mechi mbili za ugenini ambazo zinaweza kuzifanya ziendeleze moto waliouwasha au kuanza kuteremka.

Baada ya kutumia vyema mechi mbili za mwanzo nyumbani na kukusanya pointi sita, Azam FC, Biashara United, Dodoma Jiji FC na KMC zina kibarua cha kuthibitisha kuwa hazijaanza kwa nguvu za soda msimu huu.

Hata hivyo, takwimu zisizovutia na mazingira tofauti ya viwanja vya ugenini vinaweza kuwa mlima mrefu kwa timu hizo nne katika harakati zao za kuendeleza ubabe zilizouanza katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kucheza nyumbani pia.

Ukiondoa ubora duni wa eneo la kuchezea la viwanja vingi, umbali wa safari kutoka mahali zilipo, umesababisha uwepo wa idadi ya mechi chache ambazo timu iliyo ugenini kupata ushindi katika raundi hizo mbili.

Katika mechi 18 za mwanzo, ni mechi nne tu ambazo zilimalizika kwa timu iliyo ugenini kuibuka na ushindi ambazo ni Simba iliyoichapa Ihefu mabao 2-1, JKT Tanzania ikiifunga Kagera Sugar (1-0), Dodoma Jiji FC ikiilaza JKT Tanzania (1-0) na Polisi Tanzania kuizabua Namungo 1-0.

KMC inayoongoza msimamo wa Ligi, itakuwa na kibarua kigumu katika raundi mbili zijazo dhidi Mwadui FC (Jumatatu) mkoani Shinyanga, kisha Kagera Sugar (Septemba 25) mkoani Kagera.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa KMC, Azam FC iliyopo nafasi ya pili itakuwa Nyanda za Juu Kusini, ambako itaanza na Mbeya City Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Septemba 20 na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Nelson Mandela siku sita baadaye.

Biashara United iliyo katika nafasi ya tatu, inapaswa ifanye kazi ya ziada kwani Jumapili itakuwa Uwanja wa Mkapa kuvaana na wenyeji, Simba, ambao ni mabingwa watetezi wa ligi na baada ya hapo itakuwa uwanja mgumu kwa wageni wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani kuvaana na Ruvu Shooting, Septemba 27.

Dodoma Jiji baada ya kuibuka na ushindi wa mechi mbili mfululizo katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, wataelekea Kanda ya Kaskazini, ambako watacheza na Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Septemba 20, kisha kuivaa Polisi Tanzania, siku sita baadaye mjini Moshi.

Akizungumzia mechi hizo mbili za ugenini, kocha wa KMC, Habib Kondo alisema haziwapi hofu kwani ana timu nzuri na kufanya maandalizi ya kutosha akiamini matokeo ni popote.

“Jambo la msingi ni vijana kufanyia kazi tunachowapa mazoezini,” alisema Kondo.

Kocha msaidizi wa Azam, Bahati Vivier alisema wamefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mechi hizo mbili za ugenini na wako tayari kwa mechi hizo.

“Tunaelewa kwamba mechi zitakuwa ngumu na ndiyo maana tunaendelea kujiandaa. Mbeya City wamepoteza mechi mbili hivyo hawatakuwa tayari kupoteza tena dhidi yetu,” alisema Vivier.

Mchambuzi, Ally Mayay alisema katika timu zote anaipa nafasi Azam kuendelea kupata matokeo hata katika uwanjani wa ugenini katika mechi ijayo dhidi ya City.

“Ukiangalia kweli kucheza katika viwanja vya nyumbani kumezibeba timu zote kwani wanakuwa huru wakisapotiwa na mashabiki wao, lakini kwa upande mwingine hata ukiwa nyumbani bila kuwa na wachezaji wenye ubora hauwezi kupata matokeo mazuri,” alisema.

Kocha Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema anazipa nafasi Azam na KMC kufanya vizuri zaidi katika michezo yao ya ugenini mwisho mwa wiki hii kutokana na kiwango walichokionyesha katika mechi mbili zilizopita.

“KMC na Azam zimesajili vizuri, zinacheza vizuri na zimejipanga hivyo nazipa nafasi ya kufanya vizuri hata katika mechi zao za ugenini,” alisema Mzazi.

Kocha wa zamani wa Kagera Sugar, Mrage Kabange alisema: “KMC inaweza kuifunga Mwadui, lakini itapata wakati mgumu kwa Kagera Sugar, wakati Azam itakuwa na mechi ngumu kwani Mbeya City waliimarika dhidi ya Yanga, hivyo watakomaa zaidi sasa.”