Vihiga Queens yagonga Kibera Girls

Thursday March 14 2019

 

By John Kimwere

NAIROBI. MALKIA wa soka la Ligi Kuu ya Kenya (KWPL), Vihiga Queens wameigonga Kibera Girls Soccer Academy (KGSA) mabao 3-0 wakati Oserian Ladies ikivuna alama sita na kutua kileleni mwa kipute hicho.

Oserian ilitwaa usukani kwa kuiranda Kayole Starlets mabao 4-0 kisha kubeba mabao 3-0 dhidi ya Wadadia LG. Wadadia LG ilikiri kipigo hicho baada ya kudungwa mabao 7-1 na Thika Queens.

Fowadi wa Harambee Starlets, Terry Engesha aliifungia Vihiga Queens mabao yote matatu.

Catherine Wangechi, Mwanahalima Adams na Fauzia Omar wa Thika Queens kila mmoja alipiga mbili safi, nao kina Lydia Akoth na Mercy Achieng kila mmoja alicheka na nyavu mara moja.

''Tunapiga hatua vizuri ila mwaka huu mahasimu wetu wameanza kwa kasi,'' ofisa wa Thika, Fredrick Chege alisema. Nayo GASPO Women ilivuna mabao 2-0 dhidi ya Nyuki Starlets.

Oserian Ladies ina pointi saba, moja mbele ya Trans-Nzoia Falcons, Thika Queens, GASPO na Vihiga Queens kila moja tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Kwenye matokeo ya mechi nyingine, Vihiga Leeds 1-7 Trans Nzoia Falcons, Eldoret Falcons 4-1 Kisumu Allstars, Mathare Women United 1-1 Makolanders.

Advertisement