Vigogo wanateseka huko FDL

LIGI Daraja la Kwanza (FDL) imeendelea mwishoni mwa wiki huku, vigogo wakizidi kupata taabu sana baada ya vichapo mfululizo vinavyowatembelea.

Juzi iliendelea kuwa siku mbaya kwa Alliance FC baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-0 mbele ya Transit Cmp na kuzidi kuburuza mkia kwenye Kundi B linaloongozwa na Geita Gold FC iliyoichapa Arusha FC mabao 3-0 Uwanja wa Nyankumbu.

Fountain Gate imezidi kuonyesha makali yake kwa kuilaza bao 1-0 Rhino Rangers iliyokuwa nyumbani Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, huku Pamba FC ikiwa nyumbani ikibanwa mbavu ya kufungana bao 1-1 na Singida United.

Kundi A Gipco FC ikitoka suluhu na Lipuli FC huku Majimaji FC mambo yakizidi kuwaendea vibaya kwa kulala bao 1-0 nyumbani mbele ya Mbeya Kwanza na kujikita kileleni kwa alama sita huku Mawenzi ikivuna alama tatu dhidi ya African Lyon kwa kuilaza bao 1-0 mchezo uliopigwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.