Vigogo waamua kukomaa kibishi

Thursday June 27 2019

By Khatimu Naheka

WAKATI mechi za raundi ya pili za hatua ya makundi zikianza jana, mabao 27 tu yamepatikana licha ya kuongezeka kwa idadi ya mechi kulinganisha na fainali mbili zilizopita, huku vigogo vya soka Afrika vikomaa mwanzo mwisho dhidi ya wapinzani wao.

Takwimu zinaonyesha katika mechi 12 za mzunguko wa kwanza vigogo wameonyesha kutawala, huku Uganda ikiufuta machozi Ukanda wa Afrika Mashariki.

Uganda ndiyo timu pekee ya Afrika Mashariki ambayo imefanikiwa kupata ushindi katika mechi za kwanza baada ya kuichapa DR Congo mabao 2-0, huku Tanzania, Kenya na Burudani zikichemsha kwa kupoteza mechi zao.

Vigogo ambao walifanikiwa kuanza vyema ni wenyeji Misri, Nigeria, Morocco, Senegal, Algeria, Ivory Coast, Mali na Cameroon huku Ghana pekee akitoa sare.

Mpaka sasa ushindi mkubwa katika mechi hizo za kwanza ni ule walioupata Mali dhidi ya Mauritania waliposhinda 4-1.

Ushindi mwembamba zaidi ni ule wa bao 1-0 walioupata Misri, Nigeria, Morocco, Ivory Coast, huku Tunisia nao wakilazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Angola.

Advertisement

Bao la mapema zaidi ni lile la mshambuliaji Mickael Pote wa Benin akifunga dakika ya pili dhidi ya Ghana.

Katika michuano iliyopita ya Gabon 2017 mabao 12 yalipatikana kwenye mechi nane, huku zile za Guinea ya Ikweta za mwaka 2015 mechi nane za awali zilizalisha mabao 19.

Hii ni mara ya kwanza kwa AFCON kushirikisha mataifa 24. Awali yalikuwa 16.

Advertisement