Vidal ataka waifunge Real Madrid ili Barca wachekelee

Muktasari:

Arturo Vidal anaamini kukutana na Los Blancos ni kama fainali huku akiwa na matumaini kuwa chama lake Inter litatwaa pointi tatu na kufanya pande mbili tofauti za mashabiki kuwa na furaha.

MADRID, HISPANIA. KIUNGO wa Inter Milan,  Arturo Vidal  amesema kama wataibuka na ushindi dhidi ya  Real Madrid  'Los Blancos'  kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya leo Novemba 3 ni wazi kuwa utafurahisha  na  mashabiki wa klabu yake ya zamani Barcelona.

Nyota huyo wa kimataifa wa Chile ambaye aliichezea Barcelona kwa misimu miwili kabla ya kutua Italia kwa kujiunga na Inter anaufahamu vizuri upinzani uliopo kati ya miamba hiyo ya soka la Hispania.

Malengo yake amesema ni kuhakikisha anaisaidia klabu yake  kuvuna pointi tatu  pamoja na kwamba anatambua kama watapa ushindi huo kwenye uwanja wa  Alfredo Di Stefano itakuwa ni sherehe vile vile kwa mashabiki wa   Barca.

"Ni mechi ngumu na kubwa. Nimecheza soka Barcelona kwa miaka miwili na nipo tayari kwa sasa kufurahia ushindi nikiwa na Inter pamoja na mashabiki wa Barcelona," amesema Vidal.

Pamoja na hayo, Vidal hana rekodi nzuri dhidi ya Real Madrid. Aliwahi kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, 2017 wakati huo akiichezea miamba ya soka la Ujerumani, Bayern Munich.

Mchezo huo ambao ulikuwa wa nusu fainali, Bayern walichezea kichapo na hata akiwa na Barcelona, Vidal alicheza michezo miwili dhidi ya matajiri hao wa Madrid, wa kwanza kwenye La Liga ilikuwa sare huku mwingine wakipoteza.

"Ninafuraha kuwa hapa na nipo tayari kutekeleza lile ambalo kocha atapenda nifanye. Kwetu kila mchezo ni fainali kwa sababu tunatambua ugumu wa mashindano haya," amesema Mchile huyo.

Katika mchezo wa leo huenda Inter  ikakosa huduma ya mshambuliaji wao  hatari Romelu Lukaku ambaye ni majeruhi kwa upande wa Real Madrid wanafaida ya kurejea hivi karibuni  kwa Eden Hazard ambaye anatajwa kuongeza makali kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Inter na Real Madrid wote watakuwa wakiutafuta ushindi wao wa kwanza msimu huu kwenye hatua hii ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika kundi lao B linaloongozwa na Shakhtar Donetsk.

 

RATIBA KAMILI YA UEFA LEO NOVEMBA 3

Lokomotiv Moscow vs Atletico Madrid

Salzburg vs Bayern Munich

Shakhtar Donetsk vs Borussia M'gladbach

Real Madrid vs Inter

FC Porto vs Marseille

Manchester City vs Olympiacos

Atalanta vs Liverpool

FC Midtjylland vs Ajax