Vichwa vitano vyasepa Simba

Muktasari:

Simba imemkosa Makusu baada ya straika huyo aliyeitungua timu hiyo mabao mawili wakati As Vita ikishinda kwao mabao 5-0 katika mechi ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu huu, ametimkia zake RS Berkane ya Morocco.

ACHANA na habari ya pambano lao la leo dhidi Mtibwa Sugar, unaambiwa huko Msimbazi kuna vichwa vitano matata vimesepa na kuwafanya vigogo vya klabu hiyo kukuna kichwa ili kusaka mbadala wao, ili msimu ujao chama lao litishe zaidi ya sasa.

Ipo hivi. Simba ilikuwa imepanga kusajili vichwa fulani ili kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao wa michuano ya kimataifa, baadhi ikaanza kuzungumza nao, lakini baada ya mabosi hao kuchelewa kuwekana nao sawa, nyota hao wameamua kusepa kwingine.

Simba ilikuwa ikiwapigia hesabu, Jacques Tuyisenge wa Gor Mahia, Lazadius Kambole wa Zesco United yas Zambia, Yacouba Songne wa Asante Kotoko ya Ghana na Jean Makusu wa As Vita ya DR Congo, Wlater Bwalya wa Nkana FC ya Zambia, mbali na beki wa kati wa Azam, Yakub Mohammed.

Hata hivyo, Azam baada ya kusikia za chinichini kuhusu beki wao huyo kisiki, fasta wakampa mkataba na kumaliza mchezo, lakini nyota wengine watano ambao walikuwa wakipigiwa hesabu kuja kuunganishwa na Meddie Kagere wote wamesepa kimtindo.

Simba imemkosa Makusu baada ya straika huyo aliyeitungua timu hiyo mabao mawili wakati As Vita ikishinda kwao mabao 5-0 katika mechi ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu huu, ametimkia zake RS Berkane ya Morocco.

Kambole kwa upande wake naye ameamua kuachana na mipango ya Simba na awali alikiri alikuwa akishawishiwa na Clatous Chama ili kutua Msimbazi na kwenda zake Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Kuhusu Songne aliyewahi kuja na Asante Kotoko na kufunika katika mechi ya Simba Day, imekuwa ngumu kuja Tanzania kukipiga Msimbazi, baada ya klabu yake kumwongezea mkataba, kwani alikuwa pia akiwindwa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Kwa Bwalya aliyeichachafya Simba kwenye mechi ya raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa, mabosi wa Msimbazi wamechemsha baada ya kubaini haikuwa rahisi kumng’oa Nkana FC, kwani ingewalazimu kuvunja benki ili impate.

Juu ya Tuyisenge usajili wake utashindikana kwa sababu iliyoelezwa kwa aina ya washambuliaji wa Simba wanavyocheza kwa sasa wanafanana naye, hivyo kumpotezea hasa baada ya presha ya kuondoka kwa Emmanuel Okwi aliyekuwa akiwindwa na Kaizer.

MGHANA AIKWEPA

Mbali na vichwa hivyo vitano, lakini Simba pia ilikuwa ikipiga hesabu ya kumnasa beki wa Azam Yakub Mohammed, ili akaimarishe ngome yao wakitaka aungane na Erasto Nyoni, Yusuf Mlipili na Paul Bukaba, ila mabosi wenzao wakashtuka na kumzuia Mghana huyo.

Mabosi wa Azam waliamua kumpa mkataba mpya wa miaka miwili badala ya ule alionao sasa kumalizika Desemba mwaka huu na hivyo kumfanya beki huyo kulikwepa jeshi la Msimbazi ambao walivaana nao hivi karibuni na kutoka nao suluhu.

Ingawa haielezwi wazi, lakini sababu kubwa ya Simba kushindwa kumalizana na nyota hao wanaowapigia hesabu ni ishu za fedha, kwani thamani za wachezaji iliyokuwa ikiwataka ni kubwa kuliko uwezo waliokuwa nao.

Kwa mujibu wa mtandao wa transfermarket inaonyesha Tuyisenge ana thamani ya Euro 40,000 (zaidi ya Sh100 milioni), wakati Kambole thamani yake ni Euro 50,000 (zaidi ya Sh 125 milioni) huku Songne ni Paundi 68,000 (zaidi ya Sh 200 milioni).

MAGORI HUYU HAPA

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori aliweka bayana msimu ujao klabu yao itafanya usajili wa wachezaji imara wakuiongezea nguvu kikosi chaoa kutokana na mapungufu watakayoainishwa na benchi la ufundi na kazi hiyo haijaanza.

Kuhusu wachezaji hao waliokuwa wakitajwa na kisha kusepa kutua Msimbazi, Magori alisema kwamba ni tetesi tu, lakini mchezaji yeyote ambao atakuwa amependekezwa na kocha ni lazima wamchukue kwa nia ya kutaka Simba ifike mbali zaidi na ilichofanya msimu huu katika michuano ya CAF.