Vibonde watishiana nyau FDL

Saturday February 9 2019

 

By ROBERT KAKWESI, TABORA

KOCHA wa Mgambo Shooting, Gift Emmanuel amesema hakuna wanachokitaka zaidi ya pointi tatu katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza leo Jumamosi dhidi ya vibonde wenzao, Arusha FC.

Mgambo Shooting mpaka sasa iko mkiani mwa Kundi B ikiwa na pointi tano huku Arusha FC ikiwa juu yao kwa alama nane na mchezo huo utapigwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Emmanuel alisema mchezo utakuwa mgumu kwani zinakutana timu zenye upinzani mkali na zinapambana kujiepusha na janga la kushuka daraja, hivyo ni lazima washinde, ndivyo ili kuhakikisha wanapata ushindi ugenini.

Alisema kikosi chake kipo fiti na wachezaji wana morali kubwa baada ya kupata ushindi wa kwanza kwa kuitandika Transit Camp mabao 3-0.

“Tunahitaji kupambana la sivyo msimu ujao hatutakuwepo kwenye hii ligi, huu mchezo wetu dhidi ya Arusha FC ni lazima tupate ushindi ambao angalau utatupandisha juu kidogo kwenye msimamo,” alisema Emmanuel.

Kocha huyo ambaye ni mgeni kwenye timu hiyo, alikabidhiwa timu katika mzunguko wa pili na kazi yake kubwa ni kuhakikisha anaibakisha kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

“Sina muda mrefu na hii timu na nimekuja kwa lengo moja la kuhakikisha timu inabaki kwenye hii ligi,” alisema.

Advertisement