Vibonde wapiga hesabu kali Ligi Kuu

Friday May 22 2020

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Wakati leo Ijumaa, Serikali inatarajiwa kukutana na viongozi wa Shirikisho la Soka (TFF) na wale wa Baraza la Michezo (BMT) ili kujadiliana utaratibu utakaotumika baada ya  Ligi kurejeshwa, makocha ambao timu zao ziko kwenye hatari ya kushuka daraja wameanza kupiga hesabu kuzinusuru timu hizo.

Jana rais John Pombe Magufuli aliruhusu shughuli za kimichezo kuendelea nchini kuanzia Juni Mosi baada ya kusimamishwa tangu katikati ya mwezi Machi ikiwa ni hatua za kuchukuq tahadhari ya janga la corona.

Baada ya tamko hilo la rais, leo vigogo wa wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na wenzao wa wizara ya afya, sanjari na wale wa BMT watakutana ili kupanga utaratibu wa namna Ligi itakavyochezwa wakati huu ambapo kunahitajika tahadhari ya janga la corona.

Wakati kikao hicho kikifanyika, makocha ambao timu zao ziko kwenye mstari mwekundu wa kushuka daraja wameanza kupiga hesabu ya kuzinusuru timu hizo Ligi itakapoendelea siku yoyote kuanzia Juni.

Licha ya nafasi ya Singida kusalia Ligi kuu kuonekana finyu, kocha wake Ramadhan Nswanzurimo amesema kwa kipindi ambacho watapewa muda wa kufanya mazoezi ya pamoja kabla ya kurudi uwanjani atakitumia kuhakikisha hawashuki.

"Timu iko mahututi, lakini nilishasema hatujafa, tunasubiri kupewa taratibu ili kuanza mazoezi ya pamoja kuanzia leo, nitahakikisha nazitumia mechi zangu zilizobaki kubaki Ligi Kuu, hatujakata tamaa, lolote linaweza kutokea dhidi yetu," alisema.

Advertisement

Kocha wa Mbao, Mutiki Adam alisema wanasubiri muongozo wa TFF ili kuanza mazoezi ya pamoja.

"Tumeambiwa leo na Kesho tutapewa muongozo, hivyo baada ya muongozo huo tutaanza kambi kujiandaa na ligi.

"Tumesalia mechi 10, tano zikiwa za nyumbani ambazo tutapambana tuzishinde zote na hizo za ugenini tukatafute sare, matokeo ambayo naamini tukifanikiwa kuyapata tutasalia Ligi Kuu.

Kocha wa Mbeya City, Amri Said amesema hesabu yake ni kuzifunga timu ambazo pia zinaning'inia mkiani na wamebakisha mechi nazo, lakini pia kutafuta sare au ushindi kwenye mechi zao nyingine zilizosalia.

"Ligi bado ngumu, lakini sitarajii tushuke daraja, Mbeya City ya sasa ni tofauti na nilivyoikuta, tumepambana na tutaendelea kupamba, najua na mechi ngumu, wapinzani wetu wengine nao wanapambana kama sisi.

Anasema wakati wowote kuanzia sasa wataanza mazoezi ya pamoja kujiweka fiti kabla ya kurejea uwanjani kumalizia ngwe ya msimu huu.

 

Advertisement