Vibonde RBA kuvunja rekodi

Muktasari:

  • Segerea BC ambayo ni timu changa kwenye RBA imecheza michezo 13 kwenye Ligi hiyo na kupoteza ambapo inakamata mkia ikiwa na pointi 13 katika msimamo.

MECHI ya rekodi! Ndivyo itakavyokuwa leo Jumamosi wakati vibonde kwenye Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) Jogoo na Segerea BC zitakapokutana zenyewe kwa zenyewe kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, jijini humo.
Mshindi katika mchezo huo ataandika historia ya kushinda kwa mara ya kwanza tangu msimu wa Ligi hiyo kuanza.
Jogoo ambaye ana uzoefu wa kutosha kwenye Ligi hiyo amekuwa na msimu mbaya kwa kutoonja ladha ya ushindi kwenye Ligi hiyo ambayo mzunguko wa kwanza unaelekea ukingoni.
Jogoo amecheza michezo 14 na kufungwa yote kwenye mzunguko wa kwanza huku akisalia na mchezo mmoja kumaliza mzunguko wa kwanza.
Kocha wa timu hiyo, Ashraf Haruni alisema vijana wake wameanza kuonyesha uhai kwenye Ligi hiyo na anaamini watashinda mchezo huo na kufufua matumaini yao kwenye RBA.
Segerea BC ambayo ni timu changa kwenye RBA imecheza michezo 13 kwenye Ligi hiyo na kupoteza ambapo inakamata mkia ikiwa na pointi 13 katika msimamo.
Mechi nyingine zitakazochezwa leo ni Tanzania Prisons itakayocheza na Magnet, Pazi dhidi ya JKT, Vijana na Mabibo Bullets wakati kesho Jumapili Kurasini Divas itacheza na Tanzania Prisons, Pazi itaonyeshana kazi na Savio.