Viatu vya Amunike vinawatosha Stars

Muktasari:

  • Mwanaspoti linakuletea orodha ya makocha saba ambao mmoja wao anaweza kukidhi vigezo vya kurithi mikoba hiyo.

WAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likivunja mkataba na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, makocha saba wanaonekana wana nafasi nzuri ya kurithi nafasi inayoachwa na mwenzao anayeondoka baada ya mwaka mmoja tu madarakani.

Makubaliano ya kuvunja mkataba na kocha mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike yamefikiwa ikiwa ni wiki moja baada ya timu hiyo kutupwa nje ya mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 yanayoendelea huko Misri.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya makocha saba ambao mmoja wao anaweza kukidhi vigezo vya kurithi mikoba hiyo.

Peter Butler

Ni kocha Raia wa Uingereza aliyezaliwa mwaka 1966 mwenye leseni ya daraja la juu la ukocha kutoka UEFA, ambaye ana uzoefu mkubwa na soka kuanzia akiwa mchezaji hadi alipogeukia ukocha.

Amecheza jumla ya mechi 515 kwa miaka 17 alipokuwa mchezaji kwenye timu 11 tofauti zikiwamo West Bromwich Albion na West Ham huku kwenye ukocha akiwa amefanya kazi hiyo kwa miaka 21 akifundisha kwenye nchi za Uingereza, Indonesia, Malaysia, Thailand, Ghana, Botswana na Australia

Aliipandisha Botswana kwenye viwango vya ubora vya FIFA kutoka nafasi ya 120 hadi ya 87 lakini pia aliiongoza kutinga fainali ya COSAFA mwaka 2016.

Adel Amrouche

Aliwahi kutuma maombi ya kuinoa Taifa Stars lakini hakufanikiwa hivyo huu unaweza kuwa wakati mzuri kwake kutimiza ndoto yake ya kuinoa timu hiyo.

Raia huyo wa Algeria mwenye umri wa miaka 51, ana uzoefu mkubwa na soka la Afrika ambao ameupata kuanzia alipokuwa mchezaji hadi alipogeukia ukocha.

Ana leseni ya juu ya ukocha kutoka UEFA na kwa sasa anainoa timu ya MC Alger ya kwao Algeria. Timu nyingine alizowahi kufundisha ni DC Motema Pembe, Guinea ya Ikweta, FK Gänclärbirliyi, Burundi, Kenya, USM Alger na Libya.

Bobby Williamson

Raia huyo wa Scotland mwenye umri wa miaka 57 ni muumini wa soka la kushambulia na anakumbukwa kama miongoni mwa watu waliopanda mbegu ya mafanikio ya Uganda kisoka kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mafanikio yake makubwa ni kuipa Uganda ubingwa wa Kombe la Chalenji mwaka 2011 na nusura aiongoze kufuzu Fainali za AFCON mwaka 2013 lakini ilichapwa kwa mikwaju ya penalti na Zambia. Kwa sasa hana timu anayofundisha hivyo itakuwa kazi rahisi kumnasa.

Milutin Sredojevic ‘Micho’

Huyu ni kama msanifu wa soka la Uganda kwani mafanikio makubwa wanayoyapata hivi sasa ni matokeo ya mipango yake ya muda mrefu ambayo aliandaa wakati alipokuwa kocha mkuu wa timu hiyo.

Kwa sasa anainoa Orlando Pirates ya Afrika Kusini lakini mara kwa mara amekuwa kitamani kuja kuinoa Taifa Stars.

Ni kocha mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika akifundisha kwa takribani miaka 18 katika klabu za SC Villa, Saint George, Yanga, Al Hilal, Orlando Pirates na timu za taifa za Rwanda na Uganda.

Ndiye kocha aliyeiongoza Uganda kufuzu Fainali za AFCON kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri kwa miaka 38.

Sebastien Migne

Baada ya Kenya kufanya vibaya kwenye Fainali za AFCON mwaka huu huko Misri, ni wazi kwamba kibarua cha kocha Mfaransa, Sebastien Migne kipo shakani na huenda akatimuliwa.

Hata hivyo haitokuwa jambo la kushangaza kama TFF, itampa nafasi.