Vanessa awapa neno wasanii akitangazwa balozi wa Ping

Muktasari:

Vanessa aliyasema hayo muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa balozi wa kampuni ya usafirishaji kwa njia ya mtandao ya Ping ambayo imeanza kazi katika Jiji la Dar es Salaam.

Mwanamuziki Vanessa Mdee ‘Vee money’ amewataka wasanii kujiheshimu na kujitengenezea ‘brand’ ambayo ndiyo nguzo kuu ya kujiuza.
Vanessa amesema mafanikio ya msanii yanatokana na yeye mwenyewe anavyojiweka na thamani yake itapanda kulingana na atakavyoamua kutumia jina lake.
Vanessa aliyasema hayo muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa balozi wa kampuni ya usafirishaji kwa njia ya mtandao ya Ping ambayo imeanza kazi katika Jiji la Dar es Salaam.
Alisema kinachomfanya yeye kupata dili za ubalozi wa kampuni mbalimbali ni namna alivyokiweka na kuheshimu kazi yake.
“Ni muhimu kujiheshimu na kutengeneza brand kwa sababu wafanyabishara wanataka kufanya kazi na watu wanaouuzika hivyo ni muhimu kwa msanii kujitambua.
Haina maana kwamba mimi ninafaa sana hapana wao wenyewe wanaangalia wanataka kufanya kazi na nani.
Kuhusu ubalozi huo Vanessa amesema imekuwa furaha kwake kupata nafasi hiyo kwa kuwa anaamini Ping imekuja kuleta mabadiliko kwenye sekta ya usafirishaji.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo Mahmood Othman amesema tofauti na ilivyo kwa apps nyingine za usafiri hiyo imekuja kuongeza ajira kwa vijana.
“Tumeleta usafiri ambao hautakuwa na manung’uniko kwa abiria wala madereva tumefanya utafiti na kuziba mapengo yote ambayo yamekuwepo," amesema Othman.