Vanessa Mdee ajitosa Rotary Marathon

Muktasari:

Mashindano ya Rotary Dar Marathon yanafanyika kwa mara ya 10 nchini ambapo fedha zinazochangishwa zimekuwa zikitumika kusaidia huduma mbalimbali za kijamii kama vile elimu, afya pamoja na maji safi na salama

Dar es Salaam. Mwanamuziki Vanessa Mdee atashiriki mbio za Rotary Dar Marathon zitakazofanyika jijini Oktoba 14.

Vanessac Mdee ambaye ni Balozi wa mashindano hayo alisema lengo lake ni kuhakikisha mbio hizo zinasaidia kupatikana kwa kiasi kikubwa cha fedha kitakachosaidia huduma ya afya kwa akina mama na watoto kwenye hospitali ya CCBRT.

"Kwa bahati nzuri mimi nimewahi kutibiwa kwenye hii hospitali na nikapatiwa huduma nzuri na bora ambazo zilinifanya niondoke nikiwa nimebadilika na nimepona na nilipata nafasi ya kuona moja kwa moja kile wanachokifanya.

Nina imani kubwa kwamba Watanzania wengi tutajitokeza kushiriki Rotary Dar Marathon ili tuweze kuunga mkono juhudi za Klabu ya Rotary katika kusaidia kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto katika Hospitali yetu ya CCBRT hapa Msasani," alisema mwanamuziki huyo.

Mwenyekiti wa Rotary Dar Marathon, Catherinerose Barretto alisema mbio za mwaka huu zitashirikisha wanariadha kutoka Tanzania, Kenya, Rwanda, Malawi na Zanzibar.