Van Gaal alivyowapa nafasi mastaa hawa,wakatoboa

Thursday March 14 2019

 

AMSTERDAM , UHOLANZI.KOCHA, Louis van Gaal ametangaza kustaafu kazi yake ya ukocha baada ya kudumu kwenye kibarua hicho kwa miaka 24.

Mdachi huyo amezifundisha klabu tano tofauti kutoka katika nchi nne tofauti, huku akishinda mataji 20, ikiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya alilobeba akiwa kwenye kikosi cha Ajax.

Van Gaal alipita kwenye timu mahiri ikiwamo vigogo Barcelona, Bayern Munich na Manchester United. Sera za kocha huyo ni kutoa nafasi kwa wachezaji makinda na ndio maana kwenye historia yake, amewapa nafasi ya kucheza mechi zao za kwanza mastaa wengi sana.

Kuna wachezaji zaidi ya 45 na hawa hapa baadhi tu ya mastaa waliotoboa na kutamba;

Clarence Seedorf – Ajax, 1992

Kiungo, Seedorf ni mmoja wa wachezaji waliopata mafanikio makubwa kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwa sababu ndiye mchezaji wa kwanza kushinda taji hilo akiwa kwenye timu tatu tofauti. Seedorf, ambaye alishinda ubingwa wa Ulaya akiwa na Ajax, kisha Real Madrid na baadaye, AC Milan, mechi yake ya kwanza kwenye soka la wakubwa alipangwa na kocha Van Gaal huko Ajax mwaka 1992.

Patrick Kluivert – Ajax, 1994

Baada ya Ajax kufeli kwenye mpango wao wa kumsajili Ronaldo wa Brazil, kocha Van Gaal akaamua kuangalia kwenye akademia ya timu hiyo kama kuna straika na hapo ndipo alipokuja kumuibua Patrick Kluivert.

Hiyo ilikuwa mwaka 1994 na hakika Patrick alikuja kuwa bonge la staa duniani akitamba kwenye soka la Uholanzi na kwenda kutamba kwingineko ikiwamo kwenye kikosi cha Barca.

Xavi – Barcelona, 1998

Kiungo aliyekuwa akipiga pasi uwanjani kama karogwa. Xavi hakika pengo lake bado halijazibwa si kwenye kikosi cha Barcelona wala kwenye timu ya taifa ya Hispania.

Lakini, kiungo huyo wa kati anayehesabika kuwa bora wa nyakati zote mechi yake ya kwanza wakati anacheza Barcelona, timu hiyo ilikuwa chini ya kocha Van Gaal, hivyo ndiye aliyempa nafasi ya kucheza staa huyo hadi hapo alipokuja kuwa bora kabisa duniani.

Carles Puyol – Barcelona, 1999

Kuna mabeki wa kati wengi waliowahi kutokea kwenye dunia hii ya soka, lakini hakuna ubishi Carles Puyol ni mmoja wao. Akicheza soka lake kwa muda wote huko kwenye kikosi cha Barcelona hadi hapo alipostaafu, Puyol alipewa nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho cha Nou Camp mwaka 1999 ambapo kipindi hicho wababe hao wa Catalan walikuwa wakionolewa na kocha Van Gaal.

Andres Iniesta – Barcelona, 2002

Hakuna ubishi, kiungo fundi wa mpira Mhispaniola, Andres Iniesta ni moja ya wachezaji wenye kipaji kikubwa sana waliopata kutokea katika dunia hii. Katika muongo wa hivi karibuni, Iniesta alitamba kwenye soka huko Barcelona na kuwa mmoja wa wachezaji wa daraja la juu sana. Lakini, kwenye kikosi hicho cha Barcelona, Iniesta mechi yake ya kwanza alicheza mwaka 2002 kocha akiwa Van Gaal.

Víctor Valdes – Barcelona, 2002

Kipa Valdes ameacha alama zake kubwa sana huko kwenye kikosi cha Barcelona ambapo alishinda mataji ya La Liga kibao pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu.

Lakini, mechi yake ya kwanza Barcelona aliingizwa na kocha Van Gaal, ambaye alikuja kukutana naye tena huko Manchester United alikomsajili. Hata hivyo maisha ya Old Trafford hayakuwa mazuri na matokeo yake akatimkia zake Middlesbrough.

David Alaba - B. Munich, 2010

Kiraka David Alaba ni miongoni mwa wachezaji wa maana kabisa waliopewa nafasi ya kucheza kwenye vikosi vya timu ya wakubwa kwa mara ya kwanza na kocha Van Gaal. Kwa sasa, Alaba ni bonge la mchezaji, akitumika kama beki wa pembeni huko Bayern Munich, lakini akicheza kwenye kiungo katika timu yake ya taifa ya Austria. Mechi yake ya kwanza Alaba kucheza Bayern, Van Gaal ndio aliyekuwa kocha.

Marcus Rashford – Man United, 2016

Kwenye kikosi cha Manchester United moja ya alama zake bora kabisa alizoacha kocha Van Gaal huko Old Trafford ni kuwaachia mchezaji moto kabisa, Marcus Rashford, ambaye yeye alimwaamini na kumpa nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho mwaka 2016.

Van Gaal ndiye kocha aliyempa nafasi ya kucheza Rashford kwenye kikosi hicho cha Man United na tangu wakati huo mchezaji huyo amekuwa moto kabisa uwanjani.

Advertisement