VIGEZO VYA KOCHA YANGA

WAKATI makocha mbalimbali duniani wakiomba kumrithi Luc Eymael aliyetimuliwa Yanga, mkurugenzi wa mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi ametaja sifa kuu za kocha anayestahili kupewa mkataba.

Madadi, kocha wa zamani wa Taifa Stars amesema: “Kwanza ni uwezo wake, rekodi, tabia na falsafa yake iendane na ya klabu, la sivyo basi klabu ikubali kuendana na falsafa ya kocha.”

“Lakini mbali na uwezo na rekodi, wazingatie pia tabia yake, Je? itaendana na uhalisi wa mashabiki nchini na klabu ili aweze kuoana na mazingira,” alisema Madadi ambaye ni kocha wa zamani wa Simba na Kariakoo ya Lindi.

Kauli ya Madadi imeungwa mkono na katibu wa Chama cha Makocha Tanzania (Tafca), Michael Bundala pamoja na mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay ambao kwa nyakati tofauti wamesema Yanga inapaswa kuleta kocha mwenye mtazamo wa ubingwa wa Afrika. “Wasiangalie ubingwa wa humuhumu (Ligi Kuu) wa kushindana na Mbao, awe na taswira ya mashindano ya kimataifa, aje na kitu kipya sio kocha wa kuifunga Lipuli,” alisema Mayay.

Bundala alisema mbali na kigezo cha leseni ambayo inapaswa kuwa daraja ‘A’ au ‘B’, waangalie kocha kuwa ana mafanikio yapi kimataifa.

“Binafsi naona Yanga ingeajiri kocha mzawa, mbona wapo kina Mkwasa (Charles ambaye ni kocha msaidizi) na Mecky (Maxime kocha wa Kagera Sugar) wana sifa,” alisema.

“Luc (Eymael), hakuwa kocha mbaya, ameshindwa kwa kitu kidogo tu, tabia.”

Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ aliishauri Yanga kuwapa nafasi wazawa akimtaja Mkwasa, Maxime ambae yupo Kagera Sugar na Zuber Katwila wa Mtibwa Sugar.

“Nimetaja makocha hao kwa sababu timu zao hazina wachezaji wa kigeni, lakini ndizo mwiba kwa timu hizo (Yanga na Simba) kwenye mechi wanapokutana, haijalishi Katwila hakuwa na wakati mzuri ila ni kocha anaweza akafanya kitu,” alisema.

“Kama mnakumbuka timu ya Taifa ya Cameroun wakati inashiriki Kombe la Dunia ilikuwa na kocha mzawa ambaye aliichezea timu hiyo, Rigobert Song, iliweza kufanya vyema imetokana na imani kwa taifa hilo kumpa mzawa na kumuunga mkono kwa asilimia 100.

“Imekuwa kama kasumba kuona Simba na Yanga haziwezi kufundishwa na wazawa wakati sio kweli. Pia Mkwasa aliweza kufanya vyema baada ya kuondoka Mwinyi Zahera, lakini ajabu hawakutaka kumpa imani, kwanza atakuwa mzalendo wa kweli na timu hiyo.”

Naye kocha wa Biashara United, Francis Baraza alisema kinachoziangusha Simba na Yanga ni kuwaamini makocha Wazungu ambao hawana uzoefu, hivyo wanakuja kujifunzia mambo mengi katika klabu zao.

Alisema kumekuwa na tatizo kwa Afrika Mashariki na Kati kutowaamini wazawa na hilo haliishii kwa viongozi na mashabiki, bali hata wachezaji wanakuwa na matarajio makubwa kutoka kwao, akisisitiza mwisho wa siku wanaangukia pabaya na kuishia kuwafukuza.

“Wasibabaike na rangi, Yanga inahitaji kocha mwenye uzoefu mkubwa, maskauti wanatakiwa kufanya kazi yao kikamilifu, waangalie mahitaji ya timu na sio kuwachukua junior (chipukizi) wa kupatia uzoefu kwao,” alisema.

Alitoa mfano wa timu za Kenya - Gor Mahia na AFC Leopard kwamba: “Nao wana tabia hizo za Simba na Yanga, lakini inatakiwa ifike mahali ya kupigania soka la Afrika kwenda kushindana Ulaya hasa wa Kombe la Dunia.”