VIDEO: Zahera aibuka msafara wa AS Vita

Friday March 15 2019

By Thomas Ng'itu

UGUMU wa mechi ya As Vita dhidi ya simba umezidi kuongezeka baada ya makomandoo wa klabu ya Simba kuzuia msafara wa Vita wakati wakiingia uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba ndio walikuwa wa kwanza kuingia uwanjani na kuanza mazoezi yao kama kawaida.
Lakini, wakati msafara wa AS Vita ukiwa unaingia majira ya saa 12:30 jioni ilianza kuingia basi ndogo aina ya Coaster nyeupe ambayo ilikuwa imebeba wachezaji huku nyuma kukiwa na gari kubwa (Youtong) na ndipo utata ulipoanzia hapo.

Makomandoo wa Simba walikuwa wanakomaa kuingiza gari zote mbili huku wengine wakisikika wakisema kwamba gari hilo kubwa kuna mwalimu wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye pia ni Mkongo inapotoka Klabu ya AS Vita.

Coaster ya wachezaji iliruhusiwa kuingia ndani lakini gari kubwa ilikataliwa na ndipo utata ulianza baada ya makomandoo wa Simba kuanza kupishana maneno na Wacongo wanaoishi Tanzania.

Maneno yalizidi kwa pande zote mbili na ndipo Kiongozi wa Simba, Crescentius Magori alipotoka ndani na kwenda getini kuangalia msafara huo kisha akazungumza na walinzi wakafanikiwa kuruhusu msafara huo.

Baada ya gari hilo kuingia makomandoo wa Simba bado walilizonga huku wakitaka kuona nani ambaye anashuka, lakini wakati mlango unafunguliwa lilianza zogO lingine.
Zogo hilo ambalo pia kulikuwa na kurushiana maneno huku wakisisitiza kila anayeshuka lazima awe na beji inayomruhusu kuingia uwanjani.


Hata hivyo, baada ya tukio hilo walishuka viongozi sita katika gari hilo na ndipo makomandoo hao wakaanza kuwa watulivu.


Wakongo ambao wanaishi Tanzania walisikika wakisema kwamba wapinzani wao walikuwa wanajua kwamba kuna kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera.


"Zahera wapo nae kila siku lakini wanamuogopa, si anafungwa huyo Zahera," alisikika jamaa huyo na kuweka Lugha ya Kongo pamoja na Kifaransa.

Advertisement