VIDEO: Yanga kusaka rekodi ya kimataifa leo

Muktasari:

  • Yanga ikishinda mechi ya leo dhidi ya Mwadui FC basi itakuwa  imeingia kwenye rekodi ya Juventus ya Italia iliyocheza mechi 19, imeshinda mechi 17 imetoka sare mbili na inamiliki pointi 53.

JEURI ya Yanga dhidi ya watani wao wa jadi Simba ni kuwazidi pointi sita ambazo Wanamsimbazi walizidondosha dhidi ya Mbao FC iliyowafunga bao 1-0, sare na Ndanda FC, Lipuli na Wanajangwani wenyewe.

Hilo ndilo linalompa ushujaa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye katika mechi 18 kapoteza pointi mbili tu kutoka sare na Ndanda na Simba na akishinda mechi yao ya leo dhidi ya Mwadui FC, itakuwa imefikisha pointi 53 sawa na Juventus ya Italia imecheza mechi 19 ina ponti 53.

Kocha Zahera atakuwa ameacha mwiba mkali kwa Simba, iliyocheza mechi 14 mpaka sasa na inamiliki pointi 33 kuhakikisha wanashinda michezo yote ya mzunguko wa kwanza iliobakia, ili kuepuka kuongeza gepu la pointi.

Utofautiano wa pointi hizo kati ya Simba na Yanga, umemuibua aliyekuwa mwenyekiti za zamani wa Wanamsimbazi Hassan Dalali 'Mzee Dalali' kutamka kuwa bado timu yake ina nafasi ili wahakikishe hawafungwi.

"Kazi iwe moja kwa Simba iwe ni kushinda mechi zote zilizosalia kwani ili wakiingia mzunguko wa pili iwe vita nyingine ambayo huwezi kujua upande wa pili wanaweza wakateleza vipi,"anasema.

Mzee Dalali anasema Simba ina wachezaji wenye uwezo, akidai ndio maana wanafanya vizuri kimataifa "Ingekuwa timu mbovu ikingepata changamoto dhidi ya timu zenye uzoefu, hivyo kitaeleweka tu bado ngoma ni mbichi,"anasema.