VIDEO: Waziri Lugola: Kutekwa MO, watu 20 wanashikiliwa

Muktasari:

Dewji 'Mo Dewji' alitekwa Alhamisi asubuhi na watu wasiojulikana wakati akienda kufanya mazoezi kwenye gym katika hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Serikali imesema imeshtushwa na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohamed Dewji 'MO' na kwamba mpaka sasa inashikilia watu 20.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema bado jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo pamoja na matukio mengine kama hayo.

Lugola amesema matukio ya utekwaji yapo na jeshi la polisi lipo makini kuhakikisha wanadhibiti matukio hayo.

Amesema mpaka sasa bado nchi ipo salama na kwamba kufuatia kutekwa kwa MO wanawashikilia watu 20.

Aidha amesema ametoa maelekezo kwa jeshi la polisi kuhakikisha mtu yoyote anayeshikiliwa hakai ndani zaidi ya saa 24 endapo ataonekana hana hatia katika kiti anachochunguzwa.

"Tukio la kutekwa kwa MO kimetushtua sana na kwamba jeshi la polisi lipo makini na tunendelea kumtafuta na kuwatafuta wahalifu,"amesema Lugola.

Matukio yapo na jeshi la polisi tupo makini tunafuatilia na kuyadhibiti matukio yote kama haya.

"Tukio hili la MO tunawashikilia watu wasiopungua 20 tukitafuta taarifa tunazozitaka na siwezi kuwataja ni kina nani tunaowashikilia."